Dkt. Mwaisobwa Apata Ithibati Rasmi ya Uandishi wa Habari kutoka JAB


Msaidizi wa Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Hotuba, Dkt. Cosmas Mwaisobwa (kushoto), amekabidhiwa rasmi Kitambulisho cha Uandishi wa Habari (Presscard) na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula (kulia) katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu – Dodoma.

Msaidizi wa Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Hotuba, Dkt. Cosmas Mwaisobwa, amekabidhiwa rasmi Kitambulisho cha Uandishi wa Habari (Presscard) na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), leo tarehe 5 Agosti, 2025, baada ya kukidhi vigezo vya kisheria vilivyowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.

Kitambulisho hicho kimetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dodoma.

Dkt. Mwaisobwa, ambaye ni miongoni mwa wataalamu wachache nchini wenye shahada ya Udaktari wa Falsafa (PhD) katika Mawasiliano kwa Umma na Uandishi wa Habari, ameungana na Dkt. Egbert Mkoko (Mjumbe wa Bodi) na Dkt. Ayoub Chacha Rioba (Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania – TBC), waliomtangulia kupokea vitambulisho hivyo.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi kitambulisho hicho, Wakili Kipangula alimpongeza Dkt. Mwaisobwa kwa kutekeleza matakwa ya kisheria na kuwasihi waandishi wengine kufuata mfano huo kwa ajili ya kuhalalisha shughuli zao za kihabari.

“Tunaendelea kuwahimiza waandishi wote nchini kuhakikisha wanakamilisha usajili na kupata Ithibati na Vitambulisho kwa mujibu wa sheria, ili waweze kutekeleza majukumu yao bila changamoto za kisheria,” alisema Kipangula.

Kuhusu mwenendo wa maombi ya Ithibati, Wakili Kipangula alisema kuwa hadi kufikia tarehe 5 Agosti 2025, Bodi imepokea jumla ya maombi 3,200 ambapo 2,109 yameidhinishwa, 674 bado yapo katika mchakato wa uchambuzi, huku maombi 43 yakikataliwa kutokana na kutokidhi vigezo vilivyowekwa.
Kitambulisho cha Uandishi wa Habari (Presscard) hutolewa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016, inayotaka kila mwandishi kuwa na Ithibati na kusajiliwa rasmi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha taaluma ya habari na kulinda viwango vya weledi nchini.