Doumbia amchomoa Ikanga Speed Yanga

YULE bundi bado anaendelea kulia kwenye mkataba wa winga Mkongomani wa Yanga, Jonathan Ikangalombo na wakati wowote anaweza kupewa mkono wa kwaheri.

Iko hivi. Ikangalombo hatma yake ndani ya klabu hiyo bado haisomeki kutokana na hesabu tofauti za mabosi wake na benchi la ufundi la timu hiyo.

Yanga juzi usiku imemtambulisha kiungo Mohamed ‘Mo’ Doumbia ambaye anakuwa mchezaji watano wa kigeni kusajiliwa katika dirisha hili kubwa.

Doumbia anaungana na Celestin Ecua, Andy Boyeli, Lassine Kouma na Balla Moussa Conte ambapo ukiwaongeza na wale wanane waliosalia kunaifanya Yanga kufikisha idadi kamili ya wachezaji 12 wa kigeni ukimjumuisha na Ikangalombo, inaifanya timu hiyo kuwa na nyota 13 wa kigeni.

Yanga imewabakisha kipa Djigui Diarra, mabeki Chadrack Boka, Yao Attohoula, viungo Maxi Nzengeli, Duke Abuya, Pacome Zouzoua na mshambuliaji Prince Dube.

Yanga imemuita mezani Ikangalombo wakianza mazungumzo mapya ya kumsitishia mkataba baada ya winga huyo kugoma kutolewa kwa mkopo.

Mbali na kuzidisha idadi ya wachezaji wa kigeni, Yanga inapiga hesabu za kuongeza kiungo mmoja mkabaji au beki wa kati na kama wakimpata, wanataka kumtoa kwenye usajili kwa muda beki wao wa kulia Yao ambaye bado anaweza kukosa nusu ya msimu kutokana na majeraha.

“Usajili tupo hatua za mwisho, lakini si unajua dirisha halijafungwa bado kuna mambo tunayatafakari taratibu kama kuna watu tukiwapata tunaweza kuwaacha wengine,” alisema bosi huyo na kuongeza;

“Kwa sasa tunaendelea na majadiliano ya kuachana na Ikangalombo, kuna wakati tuliona kama anaweza kubaki, lakini tulipokubaliana tumpe mkataba Doumbia hapo ni wazi tulijikuta tunatakiwa kuachana naye Ikangalombo, maana tunakuwa tumezidisha wachezaji wa kigeni.

“Kuna watu tunawatafuta na kama kocha akiwapata awe mmoja basi tutalazimika kumtoa kwenye mfumo Yao ambaye ni wasiwasi kama atacheza nusu ya msimu wa kwanza, bado hajapona sawasawa.”