Na Mwandishi Wetu – Dodoma
Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mheshimiwa Giuseppe Sean Coppola, tarehe 4 Agosti 2025, amefanya ziara katika Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Majanga na Tahadhari ya Mapema kilichopo Mtumba, jijini Dodoma, kwa lengo la kujionea utendaji wa kituo hicho na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Italia katika sekta ya usimamizi wa maafa.
Katika ziara hiyo, Balozi Coppola alipokelewa na mwenyeji wake Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Bi. Jane Kikunya ambapo aliambatana na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Italia (AICS) kwa Kanda ya Afrika, Bw. Fabio Minniti, pamoja na wataalamu wa shirika hilo, Bw. Paolo Razzini na Bi. Sara Pini.
Ujumbe huo ulipata fursa ya kuona kwa karibu jinsi kituo hicho kinavyotekeleza majukumu yake ya kufuatilia matukio ya majanga, kutoa tahadhari ya mapema, na kusaidia mipango ya kukabiliana na athari zake. Kituo hicho ni miongoni mwa miradi iliyofadhiliwa na Serikali ya Italia kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mheshimiwa Balozi Giuseppe alieleza kuridhishwa na mafanikio yaliyofikiwa na kituo hicho na akaahidi kuendeleza ushirikiano na Serikali ya Tanzania ili kuimarisha zaidi mifumo ya ufuatiliaji wa majanga, mawasiliano ya haraka, na utoaji wa tahadhari kwa wakati.
“Serikali ya Italia imejizatiti kushirikiana na Tanzania katika kujenga uwezo wa kitaasisi na kiteknolojia kwa ajili ya kudhibiti majanga, kupunguza madhara, na kulinda maisha ya watu wake,” alisema Balozi Coppola.
Kwa upande wao, wataalamu wa AICS walionesha utayari wa kuendelea kushirikiana na wataalamu wa Tanzania kupitia mafunzo, uboreshaji wa miundombinu ya TEHAMA, na miradi endelevu ya kujenga jamii imara dhidi ya majanga ya asili na yale yanayosababishwa na shughuli za binadamu.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kudumisha ushirikiano kati ya Tanzania na Italia katika maeneo ya maendeleo endelevu, usimamizi wa rasilimali, na ulinzi wa maisha ya wananchi dhidi ya majanga mbalimbali.