Kocha Uganda akiri presha kuwagharimu

KOCHA wa timu ya taifa la Uganda ‘The Cranes’, Morley Byekwaso, amekiri kuwa kikosi chake kilishindwa kudhibiti presha, hali iliyowagharimu katika kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Algeria kwenye mechi ya kwanza wa Kundi C wa michuano ya CHAN 2024 iliyopigwa jijini Kampala.

Katika mechi hiyo iliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Nelson Mandela, wenyeji Uganda walionekana kuzidiwa mapema, wakiruhusu mabao matatu huku wakishindwa kujibu mashambulizi ya Algeria.

“Tulijitahidi kadri ya uwezo wetu, lakini tulikosea katika kupanga safu ya ulinzi na tukalipa gharama kubwa,” alisema Byekwaso.

Aliongeza: “Wachezaji walikuwa na wasiwasi. Hatukuweza kufanya mabadiliko ya haraka uwanjani, na presha kubwa ndiyo iliyotufanya tupoteze mchezo.”

Algeria walipata bao la kwanza kupitia kichwa cha Ayoub Ghezala, kabla ya Abderrahmane Meziane kuongeza la pili. Soufiane Bayazid alifunga bao la tatu na kuzima kabisa matumaini ya wenyeji.

Ingawa Uganda walijaribu kujibu mashambulizi kwa vipindi fulani, walikosa umakini katika umaliziaji na walishindwa kabisa kuendana na kasi ya wapinzani wao.

“Bao la kwanza lilituathiri kisaikolojia. Tulikosa nafasi, tukapoteza mipira ovyo, na tukashindwa kusimamia mchezo,” alisema Byekwaso.

Licha ya kuwa na wachezaji warefu, Uganda walishindwa kwenye mipira ya juu na walionekana kupwaya katikati ya uwanja, jambo lililowapa Algeria umiliki mkubwa wa mechi.

“Kiungo chetu kilikuwa dhaifu hatukuweza kudhibiti mpira na timu ilikuwa imetanuka mno. Tunapaswa kucheza kwa umoja na kwa urahisi,” alifafanua kocha huyo.

Hata hivyo, Byekwaso amesisitiza kuwa matumaini bado yapo kwa Uganda, ambayo ina mechi mbili zaidi za hatua ya makundi. Anaamini kuwa wachezaji wake wanaweza kurejea na kuonyesha uwezo wao halisi, endapo watasahihisha makosa mapema.

Uganda sasa wanakabiliwa na mtihani mgumu katika mechi ijayo dhidi ya Guinea  wakilenga kurekebisha makosa na kufufua matumaini katika mashindano hayo.

Kwa upande wake, kocha wa Algeria, Madjid Bougherra aliisifu timu yake kwa nidhamu ya mbinu na maandalizi bora yaliyoiwezesha kupata ushindi huo mnono.

Licha ya kucheza mbele ya mashabiki wenye hamasa kubwa wa Uganda, Algeria ilionyesha kiwango bora kilichoambatana na umiliki wa mpira, umaliziaji wa uhakika na mashambulizi ya kasi kupitia safu ya ushambuliaji.

“Huu ulikuwa ushindi mzuri. Matokeo yanaonesha kazi kubwa ambayo kundi hili limeifanya. Haikuwa rahisi tulikuwa ugenini chini ya presha lakini tuliweza kutawala kiufundi na kimbinu,” alisema.

Bao la kwanza la Algeria lilifungwa kwa kichwa na Ayoub Ghezala, kabla ya Abderrahmane Meziane kuongeza la pili kwa kumalizia kwa ustadi mkubwa. Soufiane Bayazid alifunga bao la tatu na kukamilisha ushindi wa kuvutia uliowapa Algeria nafasi ya kuongoza kundi.

Takwimu zilidhihirisha ubora wao wa asilimia 55 ya umiliki wa mpira, pasi 443 zilizokamilika kwa asilimia 81 ya ufanisi, pamoja na mashuti matano yaliyolenga lango. Zaidi ya hapo, Algeria haikupata kadi yoyote huku Uganda wakipewa tatu  za njano.

“Tofauti ilikuwa kwenye mbinu,” alifafanua Bougherra.

“Ligi yetu ya nyumbani kumalizika mapema kulitupa muda mzuri wa maandalizi. Hilo lilitusaidia kuunganisha kikosi na kukifundisha katika mazingira tofauti ya mchezo.”

Abderrahmane Meziane, aliyeibuka kuwa Mchezaji Bora wa Mechi kwa bao na pasi ya bao, ndiye aliyekuwa na jukumu la kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo huku Belhocini na Mahious wakiiweka safu ya ulinzi ya Uganda kwenye wakati mgumu.

Licha ya ushindi mkubwa, Bougherra alionekana kutobweteka.

“Bado tuna kazi ya kufanya. Tunahitaji kuboresha jinsi tunavyosimamia nafasi kati ya safu zetu. Timu zenye nguvu zaidi zitataka kutumia mapungufu hayo,” aliongeza kocha huyo.