Dar es Salaam. Katika Taifa ambalo vijana ndio kundi kubwa la watu, ajira imeendelea kuwa ajenda kuu katika kila uchaguzi mkuu. Kila mwaka, maelfu ya wahitimu kutoka vyuo vikuu na vya kati huingia sokoni kutafuta ajira, lakini nafasi hizo zimeendelea kuwa haba.
Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, vyama mbalimbali vya siasa vinaendelea kuwasilisha mikakati yao ya kushughulikia changamoto ya ajira kupitia ilani zao. Chama cha National League for Democracy (NLD) ni miongoni mwa vyama hivyo, kikiwa kimezindua rasmi ilani yake ya uchaguzi leo Jumanne Agosti 5, 2025, katika Makao Makuu yake yaliyopo Temeke jijini Dar es Salaam.
Ilani hiyo imeweka ajira kwa vijana kuwa ajenda ya kipaumbele, sambamba na mageuzi katika mfumo wa elimu kwa lengo la kujenga uchumi wa kisasa na jumuishi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, mgombea urais kwa tiketi ya NLD, Doyo Hassan Doyo amesema: “Leo tunazindua rasmi ilani yetu ambayo inalenga kufuta tatizo la ajira nchini.”
Amesema mbali na ajira, chama hicho pia kimejipanga kushughulikia masuala ya afya, miundombinu, Tehama, kilimo na ufugaji.
Mpango wa Vijana kwa Kazi
Katibu wa ilani wa chama hicho, Fahad Hassan ameainisha mikakati kadhaa ya kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana.
Miongoni mwa mipango hiyo amesema ni kuanzishwa kwa mpango wa kitaifa uitwao Vijana kwa Kazi utakaotoa mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wa vyuo vya kati na vikuu kwa kipindi cha miezi 6 hadi 12.
“Mpango huo unalenga kupunguza pengo kati ya elimu na soko la ajira, kwa kuwapa wahitimu uzoefu kabla ya kuingia kikamilifu kazini,” amesema Hassan.
Akizungumzia mageuzi ya elimu na ajira, Hassan amesema ilani yao inapendekeza mabadiliko ya mitalaa kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vikuu ikilenga kuimarisha maarifa ya vitendo, ubunifu, lugha za kigeni, Tehama na biashara.
Pia, amesema elimu ya msingi hadi sekondari na vyuo vya kati itatolewa bila malipo, huku wanafunzi wa elimu ya juu wakipata mikopo yenye masharti nafuu.
Kwa vijana wanaopendelea kujiajiri, amesema ilani yao inapendekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Taifa wa Uwezeshaji wa Vijana, utakaotoa mikopo isiyo na riba kupitia vituo vya kijana mjasiriamali vitakavyoanzishwa katika kila halmashauri.
“Vituo hivyo vitatoa elimu ya biashara, usajili wa kampuni, taarifa za soko, ushauri na huduma za kifedha, bila ada wala ushuru kwa miaka mitatu ya mwanzo wa biashara,” amesema.
Katika kuchochea ajira nje ya mfumo rasmi, NLD inaahidi kuanzisha kiwanda kimoja cha kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo au madini katika kila mkoa.
Imesema viwanda hivyo vitakuwa chanzo cha ajira kwa vijana wa vijijini na maeneo yasiyo na fursa nyingi za ajira rasmi.
Pia, imeahidi kujenga vyuo vya ufundi (Veta) hadi ngazi ya kata nchini nzima, sambamba na kutekeleza mpango kiliouita ‘Digital Youth Empowerment’ utakaoandaa vijana kwa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), biashara, ubunifu na stadi za maisha.
Akizungumza na Mwananchi, Dk Paul Loisulie, mtaalamu wa siasa na utawala bora kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), amesema mafanikio ya sera yeyote ya ajira yanategemea utekelezaji wake.
“Sera bila utekelezaji wa vitendo ni maneno matupu,” amesema Dk Loisulie.
Profesa Mohammed Makame kutoka Zanzibar amesisitiza kuwa, changamoto za ajira na elimu haziwezi kutatuliwa na wanasiasa peke yao, bali kwa ushirikiano na wataalamu, wachumi na jamii kwa jumla.
“Matatizo haya yanahitaji mkakati wa kitaifa unaovuka mipaka ya kisiasa,” amesisitiza Profesa Makame.