Mapro Simba watia neno dili la Mlingo

BAADA ya Simba kumtangaza beki mpya wa kushoto, Antony Mlingo akitokea Namungo FC, mastaa wa zamani wa klabu hiyo wamesema kocha Fadlu Davids anapenda soka la vijana na kisasa zaidi.

Mwanaspoti lilikuwa la kwanza kuripoti taarifa za Mligo aliyezaliwa Agosti 8,2007 kwamba tayari amemalizana na Simba ambayo kwa sasa imepiga kambi nchini Misri kujiandaa na msimu ujao wa 2026/27.

Usajili wa Mligo umemfurahisha beki wa zamani wa Simba, Yanga na Stars Amir Maftah aliyesema:”Simba inaonyesha mipango ya muda mrefu na mfupi, hivyo wanaposajili vijana na wakafanikiwa kucheza kwa kiwango cha juu, wakikaa kwa muda mrefu itawasaidia kujenga kombinesheni kubwa.”

Lejendari mwingine, Zamoyoni Mogella, aliyewahi kuzichezea Simba, Yanga na Stars alisema: “Kila mchezaji anapisajiliwa na timu inakuwa kwa ajili ya manufaa, kinachotakiwa kwa Mligo ajue kocha anahitaji nini kutoka kwake, asije akalewa sifa na mwisho wa siku akaishia benchi.

Aliongeza: “Kucheza Simba na Yanga ni heshima pia mchezaji anajipatia kipato ingawa kuna changamoto kwa wazawa wengi wanapenda kuridhika, ninachoshauri aige mfano wa kaka zao kama Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Shomari Kapombe na wengine ambao wanapambana na thamani zao zipo juu.”

Aliyewahi kuwa kocha na mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Abdallah  Kibadeni ‘Seif ‘King’ alisema :”Nina kituo cha soka, hivyo naamini katika vijana wakijipambanua na kujituma basi soka litabadilisha maisha yao, usajili wa Mlingo nauona ni mzuri kwa sababu ana kipaji kikubwa wanaweza wakamtumia kwa muda mrefu.”

Wachezaji wengine vijana waliyosajiliwa na Simba ni Morice Abraham mwenye umri wa miaka 21, Mkenya Mohamed Bajaber (22), Msenegali Alassane Kante (24) na Rushine De Reuck raia wa Afrika Kusini (29).