Masaibu ya wasomao vyuo na umri mdogo

Dar es Salaam. Wakati idadi zaidi ya vijana wakjiunga na elimu ya juu, wito umetolewa kwa Serikali kupitia mamlaka zake husika kuweka mkazo zaidi katika maandalizi ya kisaikolojia na kitaaluma,  kwa wanafunzi wanaotoka moja kwa moja kidato cha nne kwenda vyuo vya elimu ya juu.

Wataalamu wa elimu, saikolojia na malezi wanasema vijana hawa wengi wao wakiwa na umri kati ya miaka 16 hadi 19, hukutana na changamoto mbalimbali zinazoathiri ustawi wao kijamii, kitaaluma na kisaikolojia.

Kutokana na ukosefu wa maandalizi ya kutosha, baadhi yao hujikuta wakishindwa kuhimili mazingira mapya ya chuo, hali inayochangia kushuka kwa ufaulu au hata kuacha masomo.

Utafiti mwingi unaonesha kuwa kundi hilo huwa halijakomaa vya kutosha kukabiliana na uhuru mkubwa wa  maisha ya vyuo.

Utafiti wa mwaka 2022 uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu ‘Ustawi wa Kisaikolojia kwa Wanafunzi wa Diploma’ ulibaini kuwa zaidi ya asilimia 45 ya wanafunzi walioanza masomo ya diploma kutoka kidato cha nne, walipitia msongo wa mawazo, kuhisi kutengwa au kutothaminiwa katika wiki 12 za mwanzo chuoni.

Hali hiyo inatokana na mabadiliko makubwa kutoka mfumo wa sekondari unaowasimamia kwa karibu, kwenda mfumo wa chuo unaomtaka mwanafunzi kujisimamia katika kila eneo,  ikiwa ni pamoja na kupanga muda, kushughulikia masuala ya kifedha na kijamii.

Akizungumza na Mwananchi mmoja wa wahadhiri ambaye hakutaka jina lake linukuliwe,  anasema vijana hawa hukutana na wanafunzi wakubwa zaidi kwa umri chuoni na baadhi yao hujiingiza katika makundi yasiyo sahihi ili kuonekana wamekomaa.

“Unakuta mtu ametoka mkoa mmoja kwenda mwingine tena alikuwa kijijini halafu anapata chuo mjini,  ndiyo hapo anakutana na wengine ambao wanajihusisha na vilevi, uhusiano wa kingono usio salama au hata vitendo vya kihalifu,’’ anaeleza.

Anaongeza: “Mara nyingi haya huwatokea wale watoto wasiojitambua maana hii inatakiwa uanze kujitambua mwenyewe kabla mtu mwingine hajakufuata nyuma. Sasa kama yeye mwenyewe haelewi ni kimemleta chuoni na hapati uangalizi wa kutoka kwa wazazi ndiyo inakuwa bahati mbaya kwake,”

Wasemavyo wanafunzi wenyewe

Faisal Abdallah (18) anakiri kuwa aliingia chuo akiwa na matarajio makubwa ya maisha huru, lakini hakuwahi kufikiria kuwa uhuru huo unaweza kuwa na gharama kubwa.

Baada ya kufanya vibaya katika mitihani yake ya awali ndipo aliposhtuka na kuanza kufanya jitihada za kujinasua. Hata hivyo bado anasafisha njia yake ya elimu lakini amejifunza kwa njia ngumu.

“Nilikuwa najiona kama mtu mzima. Nilianza kupoteza mwelekeo, nikaingia kwenye makundi ya marafiki waliokuwa wakipenda starehe kuliko masomo. Nilikuwa navuta sigara, nakosa darasa, hadi nikapewa onyo la mwisho,” anasema.

Mwingine ni Anna Leonard aliyejiunga na masomo ya diploma ya uhasibu akiwa na miaka 16 mara baada ya kufaulu kidato cha nne kwa alama za juu.

Alikuwa na ndoto ya kuwa mhasibu wa kampuni kubwa ya kimataifa, ndoto hiyo ilianza kukumbwa na mawingu siku chache baada ya kufika chuoni.

“Sikuwa nimewahi kulala nje ya nyumbani, sikujua jinsi ya kupanga bajeti ya hela ya mwezi mzima. Nilikuwa nikitumia pesa yote ya matumizi wiki ya kwanza, na wiki zinazofuata napata tabu lakini baadaye nilizoea na kujipanga vyema,” anasema.

Mtazamo kisaikolojia, kimalezi

Mwanasaikolojia James Liganga anasema licha ya vijana hawa kutoka shule za sekondari wakiwa na uwezo wa kitaaluma, mara nyingi hukosa ukomavu wa kijamii unaohitajika kwa mazingira ya chuo.

“Taasisi za elimu ya juu ni maeneo yenye watu wa rika na utamaduni wa aina mbalimbali. Bila ukomavu wa kijamii, vijana hawa hujikuta katika hali ya upweke, woga wa kushiriki mijadala au hata kushindwa kujiamini,” anasema.

Liganga anasema mashinikizo ya kitaaluma yanapoongezeka kwa vijana hawa, wengi huathirika kisaikolojia, kushuka ufaulu au hata kupata matatizo ya afya ya akili.

Ili kukabiliana na hali hiyo, anashauri vyuo kutoa huduma madhubuti za ushauri  na unasihi kwa wanafunzi wapya, pamoja na kuweka mifumo ya kuwaandaa kisaikolojia na kijamii kabla na mara baada ya kujiunga na masomo.

Naye mshauri wa malezi, Petronia Daniel anasema mazingira ya chuo huwapa uhuru wanafunzi wengi, hivyo hushindwa kuutumia vyema na matokeo yake kujikuta wakipoteza mwelekeo.

“Wakiwa sekondari, wana uangalizi wa karibu wa walimu na wazazi. Lakini wakifika chuo, wanatakiwa kusimamia kila kitu wao wenyewe kutoka fedha, muda hadi uamuzi wa maisha,” anasema.

Petronia anaonya kuwa hali hii huwafanya wengine kujikuta wakichukua uamuzi usio sahihi, hasa katika masuala ya uhusiano au matumizi ya rasilimali, jambo linaloweza kuwa na athari za muda mrefu kwa maisha yao.

Mary Lawa ambaye ni mzazi anasema changamoto hiyo inachangiwa pia na vyuo kukosa utaratibu wa kuwafuatilia wanafunzi kwa kile kinachoaminika kuwa kila anayejiunga na chuo tayari ni mtu mzima.

“Mazingira ya vyuo ni tofauti na sekondari, haiwezekani mtu ambaye alikuwa anatambulika kama mtoto miezi michache iliyopita leo ghafla aingie chuo awe mtu mzima, wakati kule alikuwa anafuatiliwa hata kwa bakora huku anaachwa awe huru.

“Mwanafunzi anaamua aingie darasani au asiingie, anapata uhuru wa ghafla. Binafsi naona ipo haja ya vyuo kutenga muda katika mwaka wa kwanza kuwafundisha hawa vijana namna ya kufaulu wawapo shuleni, nini wafanye ili uwezo wao kitaalum uendelee kuwepo,”anaeleza.

Lingine analosema  linachangia wanafunzi wengi wa vyuo kushindwa kuendelea na masomo,  ni kushindwa kubadili mabadiliko wanapofika vyuoni.

Anasema: “Chuoni mwanafunzi anajipangia maisha, anakutana na uhuru wa ghafla ambao hakuupata alipokuwa sekondari, sasa kama hana control (udhibiti) anaweza kuingia kwenye makundi yatakayomfanya asahau kilichompeleka chuoni.”

Ripoti ya Tanzania Youth Development Agenda ya mwaka 2023 inaonesha kuwa asilimia 30 ya vijana wa chini ya miaka 20 wanaosoma diploma, walishawishiwa kuingia kwenye tabia hatarishi ndani ya miezi sita ya kwanza chuoni.

Akizungumzia hilo,  mhadhiri msaidizi wa Chuo cha Bahari (DMI), Eliyusta Haule anasema changamoto nyingine,  ni vijana kujiunga na kozi bila kuwa na uelewa wa kina kuhusu nini wanataka kusoma na kwa nini.

 “Unakuta mtu anachagua kozi bila kuelewa inaweza kumsaidia vipi au itampeleka wapi. Anachagua kwa kufuata mkumbo wa marafiki au shinikizo la wazazi.Hii huchangia baadhi yao kukosa motisha, kutohudhuria masomo au hata kuacha chuo kabisa,”anasema.

Taarifa ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ya mwaka 2021 ilionyesha kuwa zaidi ya asilimia 25 ya wanafunzi wa diploma walio chini ya miaka 20, walihama kozi walizoanza ndani ya mwaka mmoja wa kwanza, wakieleza kuwa hawakuzielewa vizuri kabla ya kujiunga.

Faida kujiunga umri mdogo

Hata hivyo, Eliyusta anasema zipo faida kwa  vijana kujiunga mapema na elimu ya juu akieleza kuwa kuwa kwa dunia ya sasa inayohitaji kasi na ubunifu, vijana wanaopata nafasi ya kujifunza mapema wana nafasi nzuri ya kuhimili ushindani wa maisha ya kisasa.

“Kama kijana atapata ujuzi mapema, inakuwa rahisi kwake kuanza kujitafuta na kujiondoa kwenye utegemezi akiwa bado na umri mdogo. Kinachohitajika kwa sasa sio kuwa na cheti bali  kuyatumia maarifa uliyoyapata na kuyageuza kuwa fursa,” anasema.

Hoja hiyo inaungwa mkono na Jonathan Kimario ambaye kitaaluma ni fundi umeme aliyehitimu ngazi ya diploma,  anayesema ni muhimu mfumo wa elimu ukaangaliwa upya na ngazi hiyo ikapewa kipaumbele kwa sababu ndiyo inazalisha nguvu kazi.

Kimario anasema ngazi hiyo ya elimu hasa kwa kozi za ufundi kwa kiasi fulani itasaidia kuwaondoa vijana kwenye mawazo ya kusubiri kuajiriwa badala yake watatafuta namna ya kujiajiri baada ya kuhitimu ngazi za elimu wanazopitia.

“Katika vyuo vya ufundi,  mtaalaa umeandaliwa kumwezesha mwanafunzi kujiajiri mara baada ya kumaliza mafunzo yake, kwa kuwa kule unafundishwa ufundi na namna ya kuyahamishia mafunzo hayo kwenye biashara.’’

“Hapo sasa inahitaji jitihada za mtu kwa kuwa wapo ambao wana skills (stadi) lakini hawajui jinsi ya kufanya ujasiriamali. Muhimu ni kwamba lazima ufahamu namna ya kuhamishia ulichojifunza kwenye biashara na kazi hiyo inafanyika katika vyuo vya ufundi,” anaeleza.

Pamoja na jitihada hizo changamoto inabaki kwenye mitazamo ya wanafunzi,  kwani wengi wao bado wana mawazo ya kusubiri kuajiriwa baada ya kuhitimu mafunzo yao.