WAKATI leo ikipigwa mechi mbili za kundi D, la Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN), mwitikio hadi sasa ni mdogo kwa mashabiki, licha ya nje ya Uwanja wa New Amaan Complex unaopigwa pambano hilo kuonekana shwari kiusalama.
Maeneo mbalimbali visiwani Zanzibar, shughuli za kawaida kwa maana ya za kiuchumi ndizo ambazo zimetawala, huku nje ya eneo la Uwanja wa New Amaan Complex unaotumika kwa mechi za CHAN 2024 kundi D, ukiwa katika mandhari nzuri hasa ya kiusalama.
Barabara ya kuingia geti kuu uwanjani hapo imefungwa, huku askari Polisi wakipiga doria maeneo mbalimbali ili kuhakikisha usalama unatawala kabla na baada ya mechi hizo za kundi D kupigwa.
Katika barabara hiyo ya kuingia geti kuu, gari zinazopita ni zile za askari pekee na watembea kwa mguu ila daladala zinazofanya biashara sehemu mbalimbali haziruhusiwi kusogea karibu na eneo hilo tangu saa 3:00 asubuhi njia hiyo ilipofungwa.
Hata hivyo, muitikio wa mashabiki kuingia uwanjani hapo kwa ajili ya kuangalia mechi za leo bado ni mdogo, licha ya umati wa watu wengi wanaopita nje wakienda maeneo mbalimbali kwa ajili ya shughuli zao.
Kwenye Uwanja New Amaan Zanzibar, leo zinachezwa mechi mbili za kundi D, ambapo Congo itacheza na Sudan kuanzia saa 11:00 jioni, huku bingwa mtetezi, Senegal ikipambana na Nigeria saa 2:00 usiku.