MASHUJAA imeshinda vita ya kumwania mshambuliaji Ismail Mgunda aliyekuwa akihitajiwa na Singida Black Stars na mabosi wa pande zote mbili wamefunguka kila kitu kuhusu usajili huo.
Hapo awali, Mgunda aliwahi kuichezea Singida kabla ya kutimkia Mashujaa aliyokuwa akiichezea mwanzoni mwa msimu uliomalizika kisha kwenda AS Vita ya DR Congo. Ikadaiwa alisaini Singida mara aliporejea kutoka nje ya nchi, licha ya kuwa na mkataba na Mashujaa.
Mwanaspoti linafahamu kuwa Mgunda alikuwa na mkataba na Mashujaa hadi 2028, ila alikubali ofa ya Singida jambo lililozua mvutano, huku klabu zote hizo zikidai ni mchezaji wao.
Mmoja kati ya viongozi wa Singida, aliliambia Mwanaspoti; “Tumekubaliana kumuacha Mgunda akacheze Mashujaa, tumefanya haya kwa maslahi ya mchezaji ili asipate shida ya kuja kufungiwa.
“Ni kweli tulimsainisha tena ni mara tu baada ya kurudi kutoka DR Congo, lakini unajua Singida sisi sio watu tunaotaka mivutano, tumekaa na wenzetu wa Mashujaa na kukubaliana kijana akacheze kwao, nadhani mkiwatafuta watawapa taarifa kamili.”
Kwa upande wa Mashujaa, Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Edward Swai alisema; “Ni kweli kwamba Mgunda tutakuwa naye tena msimu ujao na ana mkataba wa miaka mitatu na timu yetu hivyo bado yupo sana.
“Makosa yapo kwa wachezaji ila hayawezi kuharibu mipango ya timu, bado tupo na Mgunda na tayari tumeshafikia makubaliano na Singida, hivyo kila kitu kipo sawa,” alisema Edward aliyefichua kambi ya timu hiyo imeanza kupokea wachezaji tangu juzi jijini Dar es Salaam kabla ya kuhamia Arusha.
“Wachezaji wameshaanza kufika kambini tangu jana (juzi), hivyo tutaanzia hapa Dar es Salaam kabla ya kwenda Arusha ambako tumepanga kujiandaa na msimu mpya wa mashindano wa 2025-26.”