Mawaziri, wawakilishi Zanzibar wachemka kura za maoni

Unguja. Mchakato wa kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), huenda ukawatenganisha mawaziri na naibu mawaziri kadhaa na nafasi za uwakilishi katika baraza lijalo la wawakilishi.

Hilo linatokana na mawaziri na naibu mawaziri hao kutokuwa sehemu ya watiania wa uwakilishi walioongoza katika kura za maoni za wajumbe wa CCM.

Viongozi hao walioshindwa kuongoza katika mchakato huo ni Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis aliyewania uwakilishi katika Jimbo la Micheweni.

Wengine ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Juma Makungu Juma aliyekuwa anaomba uwakilishi wa Uzini na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Nadir Abdulatif Yussuf aliyekuwa anaomba uwakilishi wa Chaani.

Ingawa watatu hao, bado wana nafasi ya kupitishwa na vikao vya juu vya chama hicho kwa ajili ya kugombea nafasi hizo, lakini matokeo ya kura za maoni yanawatenga na nafasi hizo.

Viongozi hao, wanaungana na mawaziri wawili ambao Kamati Kuu ya CCM haikurudisha majina yao kuingia katika mchakato wa kura za maoni ambao ni Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Shaib Hassan Kaduara na Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Masoud Ali Mohamed.

Jimbo la Micheweni lilikuwa linaongozwa na Shamata Shaame Khamis ambaye ni Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo ameshindwa kutetea nafasi yake kwa mujibu wa matokeo katika ngazi hiyo ya kura za maoni.

Dk Hamad Omar Bakari ameshinda nafasi ya uwakilishi katika jimbo hilo kwa kupata kura 270 huku akimpiga chini Shamata Shaame Khamis aliyepata kura 236.

Msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Ali Suleiman Abeid amemtangaza Dk Hamad Omar Bakari kuwa kinara wa uchaguzi wa uwakilishi katika jimbo hilo.

Wengine katika mchakato huo ni Muzdalfa Ahmad Rashid amepata kura mbili, Khatib Faki Khatib kura saba kati ya 520. Kura zilizoharibika ni tano na halali zilikuwa 515.

Mwingine ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Jimbo la Uzini, Juma Makungu Juma amepata kura 205 akishindwa kutetea nafasi yake ya uwakilishi katika hatua hiyo na Badria Masoud Natai akiongoza kwa kupata kura 509.

Katibu wa Wilaya ya Kaskazini, Aziza Salum amemtaja Ali Mood Ali kwamba kapata kura 89 na Zainab Omar Ali akipata kura 46.

Mwingine ambaye ameshindwa katika kura hizo ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi katika jimbo la Chaani, Nadir Abdulatif Yussuf aliyepata kura 510 akiongozwa na Juma Usonge aliyepata kura 588.

Mbali na mawaziri hao, wawakilishi wengine ambao wameshindwa kutetea nafasi zao katika majimbo waliokuwa wakishikilia ni  Ameir Abdalla Ameir (Kwerekwe), Mohamed Ahmada Salum (Malindi), Nassor SalimAli (Kikwajuni), Rukia Omar Ramadhani (Aman), Shaaban Waziri (Uzini).

Katika majina ambayo wawakilishi hawakurudishwa walikuwa watano Jimbo la Magomeni, Jamal Kassim Ali, Jimbo la Tumbatu mwakilishi wake alikuwa Haji Omar Kheri ambaye jina lake halikurudi badala yake yamerejea Mohamoud Omar Hamad na Mtumweni Ali Saleh.

Katika Jimbo la Kiwani, Mussa Foum Mussa jina lake halikurejea badala yake limekuja jina moja la Makamu wa pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla.

Mwakilishi mwingine ambaye jina lake limeenguliwa ni wa jimbo la Mkoani Abdulla Khamis Kombo ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi.

Mwingine ambaye amekatwa ni mwakilishi anayemaliza muda wake jimbo la Chumbuni Miraji Khamis Mussa.

Wakizungumza kuhusu hatua hiyo wachambuzi wa siasa Zanzibar wamesema huo ni uamuzi wa wajumbe kulingana na wagombea walivyokuwa wakikubalika kwao.

Mchambuzi wa siasa za Zanzibar Ali Makame amesema licha ya kwamba bado ni mchakato lakini hatua hiyo inatoa taswira kamili namna gani walioshindwa kutetea nafasi zao walikuwa na upungufu kwenye maeneo yao.

“Huu bado ni mchakato, hakujawa na mshindi wa moja kwa moja kwasababu vikao vya juu vya CCM ndio vitaamua, lakini tayari inatoa picha fulani katika mazingira kama haya,”amesema Makame.

“Kikubwa katika miaka mitano wanayopewa kuongoza, wanatakiwa kujenga ukaribu kwa wapigakura, kuwapa ushirikiano, kuwatatulia kero zao lakini baadhi yao hawafanyi hivyo jambo linaloibua hisia tofauti kwa wananchi.”