KOCHA wa zamani wa Taifa Stars, Marcio Maximo ameonyesha furaha na matumaini makubwa kwa timu hiyo baada ya kuonyesha kiwango bora katika mechi ya kwanza ya Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2024 dhidi ya Burkina Faso.
Maximo ambaye kwa sasa ni kocha mpya wa KMC, alisema hana mashaka na safu ya kiungo ya Stars aliyoitaja ndio moyo wa timu, huku akiamini endapo kiwango hicho kitaendelea, Tanzania inaweza kutinga robo fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya CHAN.
“Niliona mpira wa kisasa, niliiona timu inayocheza kwa mpangilio. Lakini kiungo! Kiungo cha Taifa Stars kilikuwa na nidhamu ya hali ya juu. Ukipata kiungo chenye utulivu, kinachoweza kudhibiti kasi ya mechi, hiyo ni asilimia 70 ya ushindi,” alisema Maximo.
Maximo aliyeipeleka Taifa Stars katika CHAN ya kwanza ya mwaka 2009 iliyofanyika Ivory Coast, alisema anaguswa sana kila anapoiona timu hiyo ikifanya vizuri, kwani anaamini alishiriki kupanda mbegu ya mafanikio ya soka la Tanzania.
Katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Burkina Faso, safu ya kiungo ya Stars iliwakilishwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mudathir Yahya na Yusuf Kagoma. Wote walionyesha kiwango bora cha uelewano, nidhamu na uwezo wa kudhibiti mechi katikati ya uwanja.
Fei Toto ndiye aliyekuwa na jukumu la kuongoza mashambulizi kutoka nyuma na kuzuia mikakati ya wapinzani katika eneo la kiungo. Kagoma alisimama kama mlinzi wa kwanza mbele ya mabeki, huku akitengeneza utulivu kwa kutumia maarifa na nguvu zake.
Mudathir alionyesha uwezo wa kutuliza mechi na kutoa pasi zenye akili kwenye maeneo ya ushambuliaji.
“Hawa vijana wanaonyesha ukomavu mkubwa. Fei Toto ni mchezaji wa kipekee, ana maamuzi sahihi na hana haraka. Kagoma alinivutia sana. Mudathir ni mnyumbufu, ana uwezo wa kubadilisha hali ya mchezo kwa sekunde chache,” alisema Maximo.
Kesho Jumatano, Stars itashuka tena uwanjani kuvaana na Mauritania iliyotoka suluhu na Madagascar juzi usiku.
Ushindi wowote kwa Tanzania katika mechi hiyo unaweza kuiweka pazuri kuingia hatua ya robo fainali kwani itasaliwa na mechi mbili dhidi ya Madagascar na Afrika ya Kati zinazounda kundi B zinazocheza mechi zake Kwa Mkapa, jijini Dar es Salaam.