PALE Simba kuna staa mmoja kutoka Cameroon ambaye amesalia kwenye viunga vya Msimbazi, Leonel Ateba baada ya kuondoka kwa nyota mwingine kikosini hapo, Che Fondoh Malone aliyetimkia USM Alger ya Morocco katika dirisha la usajili linaloendelea.
Hata hivyo, kinachoelezwa ni kwamba bado chama hilo linawinda mastaa wa kusajili ingawa tayari idadi ya 12 wa kigeni wanaotakiwa kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), tayari wameshatimia.
Lakini, wakati unasoma hapa elewa kwamba kiungo mshambuliaji wa Coton Sport ya Cameroon, John Bosco Nchindo amezungumzia kuvutiwa na Simba akiitaja kuwa ni moja ya timu kubwa Afrika ambayo mchezaji yeyote anaweza kutamani kuichezea.
Bosco ambaye alihusishwa na Simba katika dirisha hili la usajili, ni rafiki wa karibu na aliyekuwa beki wa timu hiyo, Che Malone ambaye amejiunga na USM Alger ya Algeria kwa mkataba wa miaka miwili.
“Simba ni timu kubwa. Ukiangalia rekodi zao kwenye CAF, mashabiki wao na jinsi wanavyojali wachezaji wao, lazima utavutiwa nayo. Kila mchezaji angetamani kucheza hapo,” amesema Bosco.
Nyota huyo ameongeza: “Ni kweli tulizungumza. Kulikuwa na nia ya Simba kutaka huduma yangu. Tulifika mbali kwenye mazungumzo lakini hatukufikia makubaliano ya mwisho. Labda siku moja itatokea.”
Katika video iliyosambaa mitandaoni, Bosco alionekana akivaa jezi ya Simba yenye namba 20 huku mgongoni ikiandikwa Che Malone, jambo lililozua maswali mengi miongoni mwa mashabiki wa klabu hiyo kuhusu mustakabali wake.
“Ni zawadi niliyopewa na rafiki yangu Che (Malone) kabla hajaondoka. Nilipoivaa ilikuwa ni ishara ya heshima kwa yeye na klabu ambayo imemtoa,” amesema.
Kwa mujibu wa chanzo cha ndani, Simba ilikuwa na nia ya kumsajili Bosco lakini kuna mambo ambayo yalikwamisha dili hilo.
“Uongozi wa Simba ulimtaka Bosco. Mazungumzo yalikuwa ya kirafiki na ya wazi, lakini mwisho wa siku, klabu yake Coton Sport haikupunguza mahitaji yake. Simba wakajiondoa,” kimesema chanzo hicho.
Chanzo hicho kimeongeza kuwa Simba haijafunga mlango wa mazungumzo na mchezaji huyo na huenda katika dirisha lijalo la usajili ikarejea mezani na mpango mwingine mpya.