KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Sudan, Mghana Kwesi Appiah amesema ni pengo kubwa kwake katika michuano ya CHAN kutokana na kumkosa nyota wa kikosi hicho Mohamed Abdelrahman.
Appiah amezungumza hayo baada ya mechi ya kwanza ya timu hiyo dhidi ya Congo iliyoisha kwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ambayo nyota huyo alikosekana uwanjani.
“Ni pengo kubwa kwa timu na mchezaji mwenyewe. Kutokana na majeraha yake ya mguu ni ngumu kuamini kama atakuwa tena sehemu ya michuano hii,” amesema.
Appiah amesema nyota huyo ambaye ni mfungaji bora kwa msimu uliopita akiwa na Al Hilal Omdurman alipata majeraha hayo wakati wa mechi ya kikosi hicho dhidi ya Al-Merrikh.
“Kwetu kama benchi la ufundi ni jambo baya sana kwa sababu sio tu ya unahodha wake ila ubora alionao, hivyo ni ngumu lakini tutapambana na waliopo fiti kucheza kwa asilimia 100.”
Kocha Huyo amewahi kuzifundisha klabu mbalimbali zikiwemo, Asante Kotoko ya kwao Ghana na Al Khartoum ya Sudan kati ya mwaka 2014 na 2017, huku akifundisha pia timu ya Taifa ya Ghana kuanzia 2012 hadi 2014.
Kwa upande wa Abdelrahman, msimu uliopita alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mauritania ilipokuwa inashiriki Al Hilal Omdurman, ambapo nyota huyo alimaliza msimu wa 2024-2025, kwa kufunga mabao saba.