Na Diana Byera,Bukoba
Mhandisi wa TANROAD Johnston Mtasingwa ameibuka kidedea baada ya kuongoza katika kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kumpata mgombea wa ubunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Mtasingwa amepata jumla ya kura 1,408 na kuwaacha mbali wagombea wenzake zaidi ya wanne waliokuwa wakiwania nafasi hiyo.
Matokeo hayo yametangazwa na Katibu wa CCM Jimbo la Bukoba Mjini, Shabani Mdohe, ambaye alieleza kuwa wagombea wengine waliopigiwa kura ni Alex Denis aliyepata kura 804, Almasoud Kalumuna kura 640, Jamila Hassan kura 66, na Koku Rutha kura 44.
Kwa mujibu wa Mdohe, jumla ya wanachama waliojiandikisha kupiga kura ni 3,033, ambapo waliopiga kura ni 2,978, Kati ya hizo, kura 20 ziliharibika na kura halali zilikuwa 2,958.
Kura hizi za maoni ni sehemu ya mchakato wa ndani wa CCM wa kumpata mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi oktoba.