Dar es Salaam. Ukurasa mpya wa siasa za mbunge wa zamani wa Kisesa, Mkoa wa Simiyu, Luhaga Mpina unatajwa kufungukia katika Chama cha ACT- Wazalendo, huku akihusishwa na nia ya kuwania urais kupitia jukwaa hilo jipya.
Mwanasiasa huyo amewawakilisha wananchi wa Kisesa kwa miongo miwili tangu mwaka 2005 kwa nafasi ya ubunge, kabla ya jina lake kuenguliwa katika orodha ya watiania wa ubunge kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Julai 29, 2025.
Tofauti na nia yake alivyokuwa CCM, Mpina anatajwa kuingia ACT- Wazalendo na nia ya juu zaidi ya uongozi, akipanga kuwania urais, ikiwa ni moja ya sharti alilokipa chama hicho, ili akubali kujiunga nacho.
Hata hivyo, umebaki mstari mwembamba kwa mwanasiasa huyo mwenye msimamo mkali kulitimiza lengo la kugombea urais kupitia ACT-Wazalendo, kwa kuwa leo, Agosti 5, ndiyo siku ya mwisho ya uchukuaji na urejeshaji fomu ya urais katika chama hicho.
Kwa maneno mengine, Mpina amebakiwa na saa chache za kujiunga na ACT-Wazalendo, wakati huohuo achukue fomu ya kupeperusha bendera ya chama hicho katika nafasi ya urais, dhidi ya wagombea wengine akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.
Iwapo atachukua fomu hiyo ya urais, Mpina atakuwa kada wa tatu wa chama hicho, kuchukua fomu ya urais wa Tanzania Bara kupitia chama hicho, akitanguliwa na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu na Aaron Kalikawe.
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Dorothy simu yake haikupokewa na hata alipotumiwa ujumbe kwa njia ya WhatsApp alisoma bila kujibu.
Kuhusu kujiunga ACT, urais
Mwananchi limedokezwa, mpango wa Mpina kujiunga na chama hicho ulianza kusukwa kitambo, tangu ilipoonekana haendi sawa na chama chake cha CCM.
Lakini, mipango hiyo kwa mujibu wa chanzo hicho, ilipata nguvu zaidi baada ya mwanasiasa huyo kuenguliwa katika orodha ya watiania wa ubunge kupitia CCM.
Chanzo hicho, kimeeleza mwanasiasa huyo hakuwa tayari kabla, ingawa alionesha nia, lakini baada ya kukatwa akaridhia kwa sharti la kuwa mgombea urais.
“Chama tayari kilishajua mgombea wake wa urais ni Dorothy kwa upande wa bara, sasa sharti la Mpina limekuja na mambo mapya, lakini inaonekana amekubaliwa,” kimeeleza chanzo hicho.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, bado ndani ya chama hicho, kuna mvutano wa kumshawishi Dorothy aachane na nia yake ya urais ili Mpina apewe nafasi hiyo.
“Mpina aliombwa agombee ubunge kule jimboni kwake Kisesa amekataa, amesema atakatwa mapema hivyo anataka urais kwa sababu kuna malengo ya kisiasa aliyonayo,” imeelezwa.
Chanzo kingine kinaeleza, hakuna mwenye tatizo kuhusu Mpina kujiunga na chama hicho, isipokuwa wanachohofia nafasi anayoitaka.
Hofu hiyo kwa mujibu wa chanzo hicho, inatokana na kumbukumbu za hayati Benard Membe mwaka 2020, ambaye inadaiwa alijiunga na ahadi lukuki, lakini hakuzitekeleza.
Chanzo hicho kinasema mazungumzo ya Mpina na chama hicho yameendelea kwa karibu wiki moja sasa, kilichobaki ni kuyahitimisha ili utambulisho ufanyike.
Huenda leo Jumanne Agosti 5, 2025, Mpina akatambulishwa katika kikao cha kamati kuu kitakachofanyika makao makuu ya ACT Wazalendo.
Mmoja wa wajumbe waandamizi wa kamati kuu (jina limehifadhiwa) ameidokeza Mwananchi huenda katika kikao hicho wanahabari wakaalikwa kuhudhuria katika sehemu ya ufunguzi.
Hata hivyo, Mwananchi ilimtafuta Mpina kwa simu, bila mafanikio.
Alipotafutwa aliyekuwa Katibu wake alipokuwa Mbunge, Jeremiah Shillingi amesema ni nje ya mamlaka yake kuzungumzia suala hilo, hivyo atafutwe Mpina mwenyewe ndiye mwenye majibu.
“Kuhusu hilo sina mandate (mamlaka) ya kulizungumza, nipo Kanda ya Ziwa. Atafutwe Mpina mwenyewe ndio azungumze kuhusu hayo mambo,” amesema Shillingi.
Kabla ya jina lake kutopendekezwa na Kamati Kuu ya CCM kuwa mgombea ubunge, Mpina alikuwa miongoni mwa wanasiasa machachari ndani ya chama hicho.
Akiwa bungeni, amewahi kumpinga Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuhusu sakata la utoaji vibali vya uagizaji wa sukari na kusababisha achukuliwe hatua ya kusimamishwa kuhudhuria vikao vya bunge.
Hata hivyo, msimamo wa mbunge huyo uliendelea hadi kupeleka kesi hiyo mahakamani.
Mbali na hilo, Mpina amekuwa akipingana na mambo kadhaa ndani ya Serikali, licha ya kuwa mbunge wa CCM. Mwaka 2015 katika mchakato wa ndani wa CCM wa kumpata mgombea urais, Mpina alikuwa miongoni mwa makada zaidi ya 30 waliojitosa.
Mambo yalikwenda mbali zaidi hadi wakati wa ziara ya Rais Samia mkoani Simiyu, alipomkosoa mbunge huyo akidai si mwakilishi mzuri wa wananchi, anafaa kuwa mbunge wa Taifa.
Kauli hiyo ya Rais Samia ilitokana na kilichozungumzwa na Mpina alipopewa fursa ya kutoa salamu, akimwambia mkuu huyo wa nchi kuwa, kama wanaosema hadaiwi, fedha hizo azipeleke Kisesa bado wana miradi mingi ya maendeleo inayohitaji kutekelezwa.