Mpina atavyobadili upepo wa urais ACT-Wazalendo

Dar es Salaam. Mbunge wa zamani wa Kisesa, Luhaga Mpina rasmi ni mwanachama wa Chama cha ACT Wazalendo akidaiwa kubadili mwelekeo wa upepo wa urais, huku wadau wa siasa wakisema ni turufu itakayokiwezesha chama hicho kuvuna wanachama wapya.

Sambamba na kujiunga na chama hicho, Mpina amekabidhiwa fomu ya kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho, suala linalotajwa kuzua mjadala na mvutano mzito.

Katika mbio hizo za urais kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Jumatano Oktoba 29, 2025, Mpina pamoja na wagombea wa vyama vingine, atakabiliana na wagombea wa vyama vingine ikiwa atapitishwa na vikao vya juu vilivyoanza jana na kuidhinishwa na mkutano mkuu leo.

Kiongozi wa ACT  Wazalendo, Dorothy Semu akimsajili kidijitali kada mpya Luhaga Mpina hivi karibuni.



Sambamba na Mpina, Kamanda mstaafu wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jamal Rwambow naye amejiunga na chama hicho.

Tetesi kuhusu Mpina kujiunga na ACT Wazalendo, zilianza mapema baada ya jina lake kuachwa katika orodha ya watiania wa ubunge wa majimbo kupitia CCM, Julai 28, mwaka huu.

Hatua hiyo ni ukurasa mpya kwa Mpina katika maisha yake ya siasa, akifungua pazia la kuingia upinzani, lakini zaidi ni kugombea urais wa Tanzania.

Akizungumzia hatua hiyo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Dk George Kahangwa amesema iwapo Mpina atagombea nafasi hiyo anaweza kutoa changamoto kubwa kwenye kinyang’anyiro hicho, kwa sababu mbalimbali ikiwemo mazingira yanayoonekana ndani ya CCM.

“Kuna baadhi ya wana-CCM hawaridhiki na utaratibu uliotumika hadi kumpata mgombea urais, kwa hiyo tayari analeta changamoto kwamba yeye amepatikana kihalali na wana-CCM wenye mtazamo kama wa kwake wanaweza kumuunga mkono,” amesema Dk Kahangwa.


Amesema Mpina anaweza kupata waliopo ndani ya ACT-Wazalendo lakini akajikusanyia wafuasi kutoka CCM ambao hawajaridhika na mchakato ulivyoendeshwa.

“Kuna baadhi ya watu ndani ya CCM waliosukumizwa kando ikiwemo yeye mwenyewe, huenda akatumia mwaya huo kuwavuta ACT Wazalendo,” amesema

Dk Kahangwa amesema ingekuwa ni ajabu Mpina angeendelea kubakia ndani ya CCM kwa sababu Mwenyekiti wa Chama alishamwashia taa ya nyekundu kuhusu kuwania ubunge, ndio maana ameamua kutafuta jukwaa jingine.

“Kilicho bora Mpina anataka kufanya nini, kama akijipanga vizuri na akawa na sera nzuri na kuonyesha kutekelezeka kwake na uwezo wa kulitoa Taifa hapa lilipom basi naweza kusema kama si kutoa changamoto basi anaweza kufanikiwa,” amesema.

Hata hivyo, Dk Kahangwa bado anaona mazingira ya kisiasa kwa vyama vya upinzani si rafiki na yeye anaenda kukipambania chama ambacho hakijawahi kushika dola katika mazingira magumu.


“Inamuhitaji nguvu ya ziada lakini naona ni mtu anayeweza kutoa changamoto na kingine kinachompa mtaji ni mambo ambayo amekuwa akizungumza. Alifikia wakati akapeleka kesi fulani fulani mahakamani akionyesha kuchoshwa na mambo yalivyokuwa yanaenda,” amesema.

Kuhusu manufaa ya chama chake, Dk Kahangwa amesema Mpina atakiongezea ACT Wazalendo viti vya ubunge, ingawa chama hicho kina nguvu upande wa Zanzibar.

“ACT-Wazalendo kitapeleka wabunge wengi bungeni, upande wa Zanzibar au nchi nzima na mtu wa namna hiyo anaongeza hata idadi ya majimbo, kwa hiyo Mpina kama hatoupata urais anaweza kuwa na mchango wa kuongeza idadi ya wabunge,” amesema.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa amesema kuhamia upande wa upinzani ni jambo la kawaida kama ilivyokuwa akina Stephen Wasira, Edward Lowassa na Augustino Mrema, ingawa inakuwa na afya zaidi na kuonyesha vyama havipaswi kuwa juu ya masilahi ya wananchi.

“Inaweza ikaleta tafsiri kwamba vyama havipaswi kufukia mahitaji ya wananchi, lakini kwa namna moja au nyingine, havitakiwi kuwabana wanasiasa wake wanapokuwa wakitimiza majukumu yao ya kiasiasa na kidemokrasia.

“Vyama vinapaswa kuwa makini, waachwe wanasiasa wake wawe huru wanapokuwa wabunge na kwenye nafasi mbalimbali watimize kwa uhuru hasa pale mtu anapokuwa amehama kwa kuhisi alikuwa ameonewa,” amesema.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu, Juma Ramadhani amesema Mpina amejiunga na chama hicho wakati sahihi, kwani wapo katika mapokezi ya wanachama mbalimbali kutoka vyama shindani kikiwemo CCM.


“Mpina si wa kwanza kuja ACT Wazalendo, wamekuja kina Membe, lakini kwa sasa ujio wake utasaidia na kuleta joto kwenye siasa na uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba.

“Mpina ni mwanasaisa mkubwa mzoefu amekuwa waziri na mbunge anazijua vyema siasa za Tanzania. Kwa hiyo ujio wake sisi ni faida kwa chama chetu. Vyama vya ni kama timu za mpira lazima tufanye usajili, ujio wake ni usajili mzuri kwa timu yetu,” amesema.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Halima Nabalang’anya amesema ni furaha kumpokea mwanasiasa huyo mahiri na makini ndani na nje ya Bunge, kwa kuwa ana uwezo wa kusimamia misingi ya utu na uwazi bila kuhofia chochote.

“Amewapigania watu wake na kupambania masilahi ya wananchi, kinachomfanya asimame sambamba na misingi ya ACT Wazalendo,” amesema.

Hadi Mpina anajiunga na chama hicho, haikuwa lelemama, habari zinasema Alianza kushawishiwa na akaweka sharti la kuwa mgombea urais ndipo ajiunge na ACT Wazalendo.

Sharti hilo la Mpina kwa mujibu wa vyanzo kutoka ndani ya chama hicho, liliibua mvutano, hasa kutokana na chama hicho kuwa tayari kimemhakikishia kiongozi wake, Dorothy Semu kuwa ndiye atakayepeperusha bendera kwenye mbio za urais.

Ngoma ilikuwa nzito zaidi kumshawishi Dorothy aachane na nia ya urais, badala yake amwachie Mpina agombee nafasi hiyo. Ilichukua takriban saa tano za mabishano na hatimaye wakaafikiana.

Wakati kikao cha kamati ya uongozi kikiendelea katika ofisi za makao makuu ya ACT Wazalendo, nje ya ofisi mijadala ilitawala baadhi ya makada wakitaka Semu amwachie Mpina kutokana na upepo wa kisiasa uliopo.

Wakati makada hao, wakiwemo wajumbe wa halmashauri kuu wakiendelea kushangilia nje ya ofisi, idara ya uenezi ya chama hicho ikaachia picha zinazomwonyesha Mpina akiwa na viongozi mbalimbali waandamizi, akiwemo Semu aliyekuwa akimsajili kada huyo mpya.

Endapo Mpina atapitishwa na ACT Wazalendo na kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwania urais, anaingia kwenye rekodi za wanasiasa wengine akiwemo Edward Lowassa aliyejiunga na Chadema mwaka 2015 na kuwania urais kupitia Ukawa.

Katika uchaguzi huo, hayati Lowassa ambaye alikuwa waziri mkuu mstaafu alichuana kwa ukaribu na mgombea wa CCM hayati John Magufuli aliyeshinda kwa kura milioni nane dhidi yake milioni sita.

Kama hiyo haitoshi, katika uchaguzi wa mwaka 2020 aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, hayati Bernard Membe alijiunga na ACT Wazalendo na kuwania urais na baadaye chama hicho kilitangaza kumuunga mkono mgombea wa Chadema, Tundu Lissu.