Dar es Salaam. Aliyekuwa Mbunge wa Kisesa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Luhaga Mpina amejiunga rasmi na Chama cha ACT-Wazalendo.
Mpina amesajiliwa kidijitali leo Agosti 5, 2025 na Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu kuwa kada mpya ambaye anatarajiwa kuwa kwenye nafasi ya juu kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.
Mpina alikuwa ni miongoni mwa watiania wa ubunge CCM ambao majina yao hayakupitishwa na Kamati Kuu ya chama hicho kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni zilizohitimishwa jana.
Katika jimbo hilo la Kisesa, kamati kuu iliwapitisha watiania saba ambao ni Lusingi Makanda, Silinde Mhachile, Joel Mboyi, D Madili Sakumi, Godfrey Mbuga, Elias Mambembela na Gambamala Michael Luchuga waliopigiwa kura za maoni na wajumbe jana Agosti 4,2025 .
Mpina ameliongoza jimbo hilo tangu mwaka 2005 na amewahi kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira na baadaye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa miaka mitatu kuanzia 2017 hadi 2020.

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu akimsajili kidijitali kada mpya Luhaga Mpina hivi karibuni.
Mwanasiasa huyo amekuwa mmoja wa wabunge wa CCM wenye msimamo mkali dhidi ya kile wanachokiamini. Mara kadhaa ameibuka bungeni kukosoa baadhi ya maamuzi ya Serikali.
Kutokana na mwenendo wake huo, amewahi kumkosoa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuhusu sakata la sukari, jambo ambalo baadaye ilielezwa amepotosha kwa kukosa ushahidi na hivyo kuadhibiwa kutohudhuria vikao kadhaa vya Bunge.