MPINA SASA RASMI ACT WAZALENDO,ACHUKUA FOMU YA URAIS

……………………….

Mbunge wa zamani wa Kisesa, Mkoa wa Simiyu, Luhaga Mpina ni mwanachama halali wa Chama cha ACT Wazalendo na tayari ameshakabidhiwa fomu ya kugombea urais wa chama hicho.

Taarifa za uhakika ndani ya ACT-Wazalendo zinasema, mwanasiasa huyo tayari amekabidhiwa kadi ya chama hicho cha upinzani na fomu ya urais jana Jumatatu, Agosti 4, 2025.

Hatua hiyo ni ukurasa mpya wa kisiasa, baada ya CCM kulikata jina lake kati ya watiania wa ubunge wa Kisesa, kwenye mchakato wa ndani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.

Taarifa za kujiunga na ACT Wazalendo zinakuja wakati chama hicho leo, Agosti 5, 2025 kinafanya vikao vya kamati ya uongozi, kamati kuu na halmashauri kuu, kuelelea Mkutano Mkuu unaotarajiwa kufanyika kesho Jumatano, Agosti 6.

Picha mbalimbali zimemwonesha Mpina akiwa na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu akimsajili kwa njia ya kidijitali.