Dar es Salaam. Mbunge wa zamani wa Kisesa, Mkoa wa Simiyu, Luhaga Mpina ni mwanachama halali wa Chama cha ACT Wazalendo na tayari ameshakabidhiwa fomu ya kugombea urais wa chama hicho.
Taarifa za uhakika ndani ya ACT-Wazalendo zinasema, mwanasiasa huyo tayari amekabidhiwa kadi ya chama hicho cha upinzani na fomu ya urais jana Jumatatu, Agosti 4, 2025.
Hatua hiyo ni ukurasa mpya wa kisiasa, baada ya CCM kulikata jina lake kati ya watiania wa ubunge wa Kisesa, kwenye mchakato wa ndani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu akimsajili kidijitali kada mpya Luhaga Mpina hivi karibuni.
Taarifa za kujiunga na ACT Wazalendo zinakuja wakati chama hicho leo, Agosti 5, 2025 kinafanya vikao vya kamati ya uongozi, kamati kuu na halmashauri kuu, kuelelea Mkutano Mkuu unaotarajiwa kufanyika kesho Jumatano, Agosti 6.
Saa 6 mchana wa leo Jumatatu, Mwananchi limemtafuta Mpina kwenye simu yake ya mkononi na baada ya mwandishi kujitambulisha na kumweleza uwepo wa taarifa za yeye kujiunga na ACT- Wazalendo ghafla simu ilikatika.
Chanzo cha uhakika kutoka miongoni mwa viongozi wa kitaifa wa ACT Wazalendo, kimeithibitishia Mwananchi kuhusu kutua kwa Mpina ndani ya chama cha kamati ya uongozi na kwamba tayari ameshachukua fomu ya urais.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, huenda kada huyo mpya akatambulishwa katika kamati kuu au halmashauri kuu leo kabla ya mkutano mkuu kesho.
Kikao cha kamati kuu ya chama hicho kimeanza mchana huu, kikiwa kimechelewa kutokana na mvutano uliokuwepo kati ya aliyepangwa awali kuwa mgombea wa urais wa ACT Wazalendo ambaye pia ni Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu na viongozi wengine.
Chanzo hicho kinaeleza, Dorothy alikuwa anashawishiwa kuachia urais kwa Mpina, au awe tayari kusimama naye ndani ya chama hicho, jambo ambalo haijafahamika limeamuliwaje.

“Bado alikuwa anashawishiwa akubali lakini amekataa kuachia urais na anasema waende kwenye kura za maoni lakini bila ushindani wa Mpina. Anasema akiwekewa Mpina kama mpinzani wake kwenye kura za maoni, atajiuzulu nafasi zote za uongozi ndani ya chama,” kimeeleza chanzo hicho.
Chanzo kingine kutoka miongoni mwa viongozi wa kitaifa wa chama hicho, kimesema wajumbe wengi wanaonekana kuvutiwa na Mpina awe mgombea urais wa chama hicho, wakimwona turufu kwa upinzani.
Kutokana na hali hiyo, chanzo hicho kimesema kikao cha kamati kuu kinaendelea kuchelewa, lakini muafaka utapatikana, kwa sababu kinachoangaliwa ni masilahi ya chama so mtu binafsi.

Chanzo hicho kimekwenda mbali na kueleza, wanaamini nyuma ya msimamo wa Dorothy, wapo vigogo kutoka ndani na nje ya chama hicho wanaosimama naye.
Hivi sasa wajumbe wapo wa kamati kuu na halmashauri kuu wapo nje wakisubiria kikao cha uongozi kimalizike, ili waingie kwenye majukumu mengine.
Nje ya ofisi za ACT wajumbe na makada wako katika makundi wakijadiliana baadhi wakisema bora Semu aachie nafasi ya urais ili Mpina agombee huku wengine wakisema waachwe wote waingie kwenye mchakato ili mkutano mkuu wa kesho uamue.
Hata hivyo, mwingine amesisikika akisema “tunafanya haya ili kuweka mambo sawa, hatutaki Semu aingie kwenye mchakato wa kura ili apate aibu mbele ya mkutano mkuu,” amesema.
Hata hivyo, baadaye Mwananchi iliarifiwa kuwa, Dorothy ameridhia kuachia nafasi ya kuwania urais na hivyo, rasmi Mpina atasimama kupeperusha bendera ya chama hicho katika wadhifa wa urais.
Jitihada za kumpata Semu tangu jana zinaendelea.
Endelea kufuatilia Mwananchi