KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’, Jacob ‘Ghost’ Mulee amefichua sababu mbili zilizomfanya Mohamed Bajaber kuachana na kikosi hicho katika CHAN na kusaini mkataba na miamba ya soka nchini, Simba.
Akifanya mahojiano na Habari 254tv ya kwao Kenya, Mulee alikiri kutokuwepo kwa Bajaber kambini kutaleta mabadiliko kadhaa, lakini Harambee Stars italazimika kusonga mbele na kuonyesha uwezo katika mashindano.
Bajaber, aliyekuwa anasumbuliwa na majeraha wakati akiwa kambini na timu hiyo, alisaini mkataba Simba na kutambulishwa siku chache kabla ya mashindano kufungulia Agosti 2 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.
Kwa mujibu wa Mulee, nyota huyo hakuwa na mchango mkubwa kwenye timu kutokana na majeraha, hali iliyomfanya kocha Benni McCarthy amruhusu aondoke kambini.
Mulee alisema kama Bajaber angeamua kubaki kambini bila kucheza thamani yake kama mchezaji ingeweza kushuka.
“Kuondoka kwa Mohamed Bajaber katika kikosi kutaathiri Harambee Stars bila shaka, lakini huwa tunasema hakuna mchezaji asiyeweza kubadilishwa kwa sababu huwezi kumtegemea mchezaji mmoja kila mara,” alisema.
“Kuna taarifa kwamba hakuwa fiti asilimia mia hivyo hangeweza hata kuisaidia Harambee Stars kwa njia yoyote kwa sababu hata wakati Kenya Police walipokuwa wakitwaa ubingwa wa ligi hakuwa akicheza.
“Nimeelewa kuwa Benni alimruhusu aondoke kwa kuwa hata CHAN hakuwa kwenye mipango ya kucheza. Natamani apone haraka na kurudi kuwa fiti.”
Mulee aliongeza kuwa ni ndoto ya kila mchezaji kupata fursa bora zaidi na uhamisho wa Bajaber kwenda Simba unakuja na faida kubwa kifedha.
Kocha huyo wa zamani wa Tusker alibainisha sababu kuu mbili za nyota huyo kujiunga na Wekundu wa Msimbazi kabla ya kuanza kwa CHAN.
Harambee Stars ilianza kampeni yake katika mashindano hayo kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya mabingwa mara mbili – DR Congo, mchezo ambao ulipigwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Moi Kasarani jijini Nairobi.
Pia alisisitiza kila mchezaji hutamani kupiga hatua kubwa zaidi na Bajaber kijiunga Simba SC ni hatua nzuri kiuchumi, wakati ikiripotiwa kuwa amesaini mkataba wa miaka miwili, huku Kenya Police wakipokea dola 100,000 sawa na Ksh12.9 milioni, pia Sh250 milioni za Kitanzania kama ada ya uhamisho.
“Nadhani kila mchezaji ana ari fulani, na huenda aliona kwamba kwenda Simba SC ni fursa nzuri, na pia alizingatia thamani ya kifedha”.
“Kama anaenda Simba na anapata pesa nzuri, na Kenya Police FC wamekubaliana na hilo, basi ni sawa, ila najua atakuja kucheza hata Ligi za barani Ulaya siku moja”, aliongeza.
Bajaber tayari ameungana na kikosi cha Simba SC kilichoko nchini Misri kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya msimu mpya 2025/26.