Kocha Mkuu wa Congo, Barthelemy Ngatsono amesema licha ya timu hiyo kuanza na sare katika michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), lakini amefurahishwa na viwango vilivyoonyeshwa na nyota wa kikosi hicho.
Kauli ya Ngatsono imejiri baada ya timu hiyo kuanza michuano ya CHAN kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Sudan katika mechi ya kundi D iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mechi hiyo, Ngatsono amesema mpira wa miguu una matokeo ya aina tatu, ingawa lengo la kila mmoja ni kuhakikisha anashinda.
“Kuna kushinda, sare na kupoteza na yote ni matokeo ya mpira wa miguu, hivyo tunafurahi kupata angalau pointi moja kwa sababu kila mmoja ameona ubora wa wapinzani wetu,” amesema Ngatsono.
Amesema kwa sasa malengo ya timu hiyo ni kuelekeza nguvu katika mechi ijayo dhidi ya Senegal ambayo anaamini itakuwa ngumu zaidi kutokana na mahitaji ya kila upande.
“Kila hatua ni ngumu na wapinzani wetu wamejipanga pia. Tumeanza kwa sare, lakini haijatuharibia malengo yetu huko mbeleni, hivyo acha tuone.”
Congo itapambana na Senegal Agosti 12, ambapo kikosi hicho kinashuka kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar saa 2:00 usiku huu kupambana na Nigeria katika mechi ya kwanza ya ufunguzi wa kundi D.