Polisi sita mbaroni wakihusishwa na kutoweka kwa bodaboda

Dar/Mikoani. Mambo mapya yamejitokeza kuhusu tuhuma zinazowakabili baadhi ya askari polisi, wakiwemo wa Kitengo cha Intelijensia mkoani Kilimanjaro, wanaodaiwa kukamatwa kuhusiana na kutoweka kwa mshukiwa wa uhalifu ambaye mwili wake haujapatikana.

Taarifa zinaeleza kuwa askari hao walikamatwa kufuatia uchunguzi ulioanzishwa baada ya kupotea kwa Deogratius Shirima (35), dereva maarufu wa bodaboda mjini Moshi, ambaye alitoweka ghafla Julai 21, 2025, muda mfupi baada ya kuagana na mkewe.

Wiki moja iliyopita, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alithibitisha kwa Mwananchi kuwa Jeshi la Polisi limepokea taarifa za kutoweka kwa Deogratius Shirima (35), dereva maarufu wa bodaboda mjini Moshi, na kwamba uchunguzi wa kupotea kwake umeanza rasmi.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwananchi imezipata kutoka Dodoma, Dar es Salaam na Moshi, zinadai kuwa Shirima alitoweka ghafla Julai 21, 2025, muda mfupi baada ya kuagana na mkewe.

Katika tukio hilo, inadaiwa kuwa baada ya mtuhumiwa kuteswa na kupoteza maisha, wahusika walikubaliana mwili wa marehemu utupwe na mmoja wao alipewa jukumu la kwenda kuitelekeza pikipiki yake.

Hata hivyo, kwa tamaa binafsi, hakutekeleza agizo hilo bali aliichukua na kuihifadhi nyumbani kwake.

Kitu ambacho askari huyo alikuwa hajui ni kuwa pikipiki hiyo ilikuwa imefungwa kifaa cha ufuatiliaji cha Global Positioning System (GPS), ambacho kiliwaongoza wamiliki wake pamoja na ndugu wa marehemu hadi mahali ilipohifadhiwa, walipochungulia dirishani waliiona pikipiki hiyo.

Taarifa kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dodoma na Dar es Salaam zinaeleza kuwa ofisa mwandamizi wa jeshi hilo amefika Moshi kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo na tayari askari sita wamekamatwa, wakiwemo wanne wa Kitengo cha Intelijensia na wawili wa Upelelezi.

Vyanzo vya kuaminika Dodoma na Dar es Salaam, vimeeleza askari hao walikuwa wanashikiliwa katika vituo vya polisi vya Same, TPC, Majengo na Rombo mkoani Kilimanjaro na moja ya vituo vilivyopo jijini Dar es Salaam.

Jioni ya leo Jumanne, Agosti 5, 2025 Mwananchi limemtafuta RPC Maigwa kwa simu na alipoulizwa juu ya tukio hilo na askari wangapi wanashikiliwa amesema: “Kama tulivyosema uchunguzi unaendelea, viongozi wakubwa tupo nao hapa.” Hata hivyo, hakufafanua zaidi viongozi hao ni wapi.

Mazingira ya tukio hilo yanataka kufanana na tukio la mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis Hamis, mkazi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi la Januari 5, 2022, yaliyotokea ndani ya Kituo cha Polisi Mitengo, Wilaya ya Mtwara.

Katika tukio hilo, askari sita walikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji hayo, lakini wawili ndio waliopatikana na hatia na kuhukumiwa adhabu ya kifo katika hukumu iliyotolewa Juni 23, 2025 na Jaji Hamidu Mwanga wa Mahakama Kuu.

Waliohukumiwa adhabu hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Mtwara (OC-CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilibert Kalanje na aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Onyango.

Taarifa ambazo Mwananchi limezipata kutoka vyanzo mbalimbali vya kuaminika, askari hao wa intelijensia wakiwa na gari aina ya Toyota Noah, walimkamata bodaboda huyo wakimtuhumu kuwa msambazaji wa mirungi mjini Moshi.

Inadaiwa askari hao walimpa kipigo wakimshinikiza atoe siri za mtandao mzima wa mfanyabiashara mkubwa anayeingiza nchini mirungi hiyo kutoka Kenya.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, baada ya kumkamata, walitoa taarifa tofauti kuwa anajihusisha na ugaidi na mmoja akapewa kazi ya kwenda kuitelekeza pikipiki lakini kwa tamaa zake akaificha ili baadaye aimiliki au aiuze,” kilidai chanzo chetu.

“Sasa hawakujua ile pikipiki ina GPS. Kwa hiyo taarifa zikamfikia mwenye pikipiki wakaanza kuitafuta ndio kuikuta nyumbani kwa askari kambini kule line polisi,” kilidai chanzo hicho na kudai kuwa wahusika walifanya kila njia kuficha.

Taarifa nyingine zinadai wahusika walitumia ujanja wa kuwatoa wahusika mahali ambapo pikipiki ilipokutwa, ili waweze kuihamisha lakini kulikuwa na kijana aliyekuwa ameachwa kuilinda, aliyetoa taarifa kuwa inataka kuhamishwa.

“Miongoni mwa askari wanaodaiwa kukamatwa ni pamoja na yule ambaye alikwenda kituoni kuomba pingu na ndiye alikwenda kumfunga kamba yule kijana aliyeachwa alinde ile nyumba ambayo pikipiki ilikutwa pamoja na wale waliomkamata,” imedaiwa.

Polisi hao inadaiwa walimkamata kijana huyo, kumfunga pingu na kumsukasuka na kumuondoa eneo hilo na wao kupata mwanya wa kuiondoa pikipiki hiyo na kwenda kuitelekeza eneo lingine.

Pikipiki hiyo inasemekana imepatikana na ipo kituo cha polisi.

Kulingana na vyanzo hivyo, kulikuwepo na jitihada na nguvu kubwa za kuficha suala hilo huku vikao siri vikifanyika kupoteza ushahidi, lakini ofisa aliyetoka makao makuu alivuruga mipango hiyo.

Ni ofisa huyo ndiye aliyetoa amri ya kukamatwa wote walikuwa zamu siku hiyo, pamoja na yeyote aliyeshiriki kwa namna moja au nyingine katika tukio hilo na kuwatawanya katika mahabusu tofauti ili wasipate nafasi ya kufundishana.

Mke wa dereva wa bodaboda huyo, Mariam Abdi alidai alipoteza mawasiliano na mumewe baada ya kuachana naye saa 11 jioni na tangu wakati huo, simu yake ikawa haipatikani hadi pikipiki yake ilipokutwa nyumbani kwa askari.

“Siku ya Jumatatu Julai 21, 2025 aliamka asubuhi, akikesha huwa anapenda kulala mpaka mchana ndio anaamka, alivyoamka kwenye saa 11, akaniambia nenda kasuke akanipa Sh11,000, nikaenda kusuka akaniletea pesa pale saluni.

 “Akaniambia baada ya dakika tano unipigie nitakuletea hela ya kupika. Nikamwambia sawa. Nilivyomaliza kusuka nikaanza kupiga simu yake haipatikani. Nikapiga karibia saa nzima haipatikani. Mpaka saa 2 usiku haipatikani.

“Mpaka saa 5 usiku nikawaambia wenzangu mbona leo mume wangu hapatikanai shida ni nini. Nikawaambia twende kwenye vijiwe tumtafute. Ana vijiwe kama vitatu. Tukaenda vile vijiwe vyote wakasema leo (Julai 21) hawajamuona kabisa”

“Tukarudi nyumbani. Ilipofika saa 7 roho yangu ikawa haina amani, nikaamua kumpigia simu rafiki yake nikamwambia kama anafahamiana na polisi aulizie kama amekamatwa amewekwa mahabusu. Akapiga simu akaambiwa hayupo”

“Nikaamua kulala hadi asubuhi nikawa siamini. Nikarudi tena vijiweni wakasema hawajamuona tangu ile jana yake. Ilipofika saa 9, nikaamua kwenda polisi, nikatoa taarifa wakaniambia mpaka saa 24 zipite ndio nirudi,”alisema Mariam.

“Ilipofika saa 11 nikarudi polisi ndio wakanipa RB namba nikarudi nyumbani. Nikaona akili hainipi kabisa nikaamua kurudi kwa bosi wake, nikamweleza mume wangu tangu jana amepotea, haonekani wala hapatikani kwenye simu.”

Mariam anadai alimshauri bosi wa mumewe ajaribu kufuatilia kwa GPS na yeye akawaacha waendelee kuitafuta na ndipo baadaye bosi wa mume wake alimpigia simu na kumwita, akisema pikipiki wameipata.

“Nikamwambia kama ana kifaa kwenye hiyo pikipiki umefunga basi jaribu ku track (kufuatilia) kama utampata, maana hapo pikipiki itakapokuwepo na yeye atakuwepo. Akaanza ku track wakaiona iko polisi ndio akaniita, ‘njoo’.

“Kaniambia pikipiki iko hapa kwa askari. Nikaenda hapo akaachwa kijana mmoja achunge. Tulipomuacha pale kumbe wakaanza (polisi) kumpiga,” alidai.

Ramadhan Singe, ndiye inadaiwa aliachwa kuchunga pikipiki ile isitolewe katika nyumba hiyo ya askari wakati bosi wake akienda kuchukua askari kituoni, lakini alishangaa walikuja askari wawili ambao walimsukasuka na kumuondoa.

“Sisi tulitoka msikitini na sheikh wangu tukaenda eneo ambalo wali track hiyo. Kufika pale wakawa wameshawasiliana na polisi wakaambiwa wakachukue askari,” alidai.

“Mimi nikaachwa pale eneo la tukio niwe kama naangalia ule mlango usiwe unafunguliwa wakatoa kile chombo pale. Baadaye akatokea askari mmoja pale Line Polisi akaniambia wewe kijana unafanya nini hapo”.

“Akaniambia hili ni eneo la maaskari haparuhusiwi kupaki hivi. Sogea mbele. Nikajiongeza nikasogea mbele. Ile kusogea mbele akatokea askari mwingine. Yule mwingine akaniambia dogo mbona kama unazurura hapa,” alidai.

“Hebu lete ufunguo wa pikipiki yako. Akaninyang’anya ufunguo wa pikipiki. Yule mwingine naye akawa amefika. Wakanipiga mtama wakanifunga pingu. Akaniambia wewe dogo ni mzururaji ni kibaka. Twende tukupeleke polisi,” amesema.

“Wakanitoa eneo lile pale wakanipeleka kama wananipeleka polisi. Wakawa wanapeana ishara wenyewe. Wakawa wanapeana ishara na simu kuwa toeni hiyo pikipiki hapo ishakuwa ni msala.

“Wakanitoa pale wakawa wananipeleka kambini kwao wanapofanyia mazoezi. Tukaanza kuvutana vutana pale. Sasa wakati tunafika barabara ya lami kule. Polisi mmoja akaniambia wewe dogo kwanza bosi wako ni yupi,” alieleza kijana huyo.

“Ile tu anaongea vile bosi wangu aliyeenda kuchukua kuchukua maaskari, akawa amepita na gari lake nikamwambia ni yule pale nyuma, kulikuwa na maaskari. Wakanizuia wakawa kama kunikinga vile. Wakawa wameshapita bosi hakuniona,”

“Wakaulizana funguo za pingu ziko wapi tumfungue huyu dogo aondoke zake. Yaani kule tayari walikuwa wameshachora mchoro pikipiki imeshatoka kule. Saa hiyo mie wamenibana. Ukaletwa ufunguo wa pingu akanitoa zile pingu walizonifunga,” amedai.

Kijana huyo alidai kuwa baada ya hapo polisi mmoja akamwambia “Sasa dogo sikiliza sisi tunakuachia, tunakupa kila kitu chako ila uende nyumbani,” na asifuatilie yasiyomhusu.