Profesa Mosha amtaja binadamu hatari sana

Arusha. Tafakari yangu ya leo itajikita katika mawazo ya watu wawili ambao ni Muft Ismael Menk na mwanamama Louise de Marillac.

Muft Menk amesema: ‘’Moyo wangu una thamani hivyo kwamba hauwezi kuipa nafasi chuki na wivu ndani yake. Na mwanamama Louise de Marillac ameandika: ‘’Kama moyo wako haukujaa joto la upendo, wengine kando yako watakufa kwa baridi.’’

Msingi wa hoja hizi mbili ni hali ya moyo wa mtu: kwa upande mmoja yaweza kuwa na upendo wa dhati kwa wengine, na kwa upande mmoja moyo wa mtu waweza kuwa hatari ya kutisha kwa wengine.

Wote wawili wanasisitiza kwamba kwa asili mioyo yetu inapaswa kujaa upendo kwa wengine, si chuki na wivu. Mioyo yetu kwa asili inapaswa kufurika joto la upendo kwa wengine, la sivyo hao wengine tutawaua kwa ubaridi wa mioyo yetu.

 Hizi hoja mbili za hawa wabobezi wa elimu ya kiroho au tuiite kwa maneno rahisi elimu ya utu, zinanikumbusha maneno ya Maandiko matakatifu yasemayo: sisi binadamu tumeumbwa kwa mfano na sura ya Mungu.

Kama ni hivyo, nami naamini kwamba hili ni la kweli, binadamu asipokuwa na hiyo sura ya Mungu ndani yake, huyo atakuwa si binadamu tena, ni shetani.

Hakuna aliye katikati ya hawa wawili: au mtu ana sura ya Mungu ndani yake, na hivyo moyo wake umejaa utu na upendo kwa wengine, au moyo wake umejaa chuki, wivu na ubinafsi.

Pia katika lugha ya wazazi wangu kuna msemo huu: mashetani ni watu. Wana maana ya kusema: tusije tukasingizia kwamba wapo mashetani nje ya ubinadamu wetu, mashetani ni sisi wenyewe.

Yaani mtu ana mawili: ama awe na sura ya Mungu, au awe shetani kwa matendo yake ya chuki, ukatili, ubinafsi na kadhalika.

 Hii ni tafakari yangu, na wewe una haki ya kuwa na ya kwako pia. Tuna uhuru wa mawazo na uhuru wa kuabudu na kuamini kile tunachodhamiria.

Tukirudi katika hoja ya msingi leo, tunaona kwamba binadamu ameumbwa ili achague kuwa na sura ya Mungu au sura ya shetani.

Au ajae utu, upendo na ukarimu kwa wengine, au awe na moyo wa jiwe uliojaa ubinafsi, uchoyo, wivu na ukandamizaji wa haki za wengine.

 Inakuwaje mtu awe na moyo wa ubaridi kiasi cha kuwaua wengine? Tunafikiaje hali hii? Hapa ndipo tunaona umuhimu wa malezi sahihi kwa watoto na kwa jamii.

Tunasema mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Mtoto akizungukwa na utu, upendo, heshima, ukarimu na kadhalika, yeye atakuwa hivyo. Tabia ya umimi na ubinafsi ikidhibitiwa tangu utotoni, basi mtoto atajijengea moyo wa ukarimu na upendo kwa wengine. La sivyo ataanza kujijengea moyo baridi ambao utakuwa kifo kwa wengine.

Tumeanza na kichwa cha habari kwamba binadamu anaweza kuwa mtu hatari sana kwa wengine. Kwa mazingira yangu hapa ninapoishi, hatari kubwa ninayoiona si simba, fisi, na chui, hatari kubwa ni binadamu kama mimi.

Hapa nchini kwetu na pengine duniani tunashuhudia ukatili usioelezeka ukitokea kila siku.

Tumezoea kusikia habari za kutisha mara nyingi hivyo kwamba tunafikia mahali tunaona kwamba haya ni matukio ya kawaida. Wanasaikolojia wanatuambia kwamba mtu akisikia habari fulani mara nyingi sana, tuseme ni habari za ubakaji, inafikia mahali anaanza kuona kwamba hilo ni jambo la kawaida, na moyo wake unaanza kupoteza uwezo wake wa kuona na kulaani uovu.

Huenda tumefikia hapo sasa. Tunasikia mauaji ya watoto huko Gaza mara nyingi hivyo kwamba tunaanza kupoteza uwezo wa kuona mateso yao.

Tunasikia kila siku matendo ya watu kuteswa na kuuawa, matendo ya wizi na ubakaji hadi mioyo yetu inapoteza uwezo wa kuumwa na uovu kama huo.

Haya yananifanya niamini kwamba kweli moyo wa mtu usipojaa upendo, basi wengine watauawa kwa baridi itokanayo na moyo huo. Wengine watatekwa, watateswa, watauawa, kutokana na ubaridi wa mioyo ya watu ambao mioyo yao haina joto la utu na ubinadamu. Ndiyo maana nasema kwamba binadamu anaweza kuwa kuwe kiumbe hatari sana kwa wengine.

Lakini tusisahau kwamba kweli wapo watu mithili ya malaika kati yetu. Wamekuwepo watu wa aina hii katika zama zote, wapo hata sasa, na watakuwepo siku zote.

Hawa ndio watu wanaotupa tumaini kwamba kuishi kuna maana. Hawa ni wale mioyo yao imejaa joto la upendo, wana utu, wanajitahidi kuwainua wengine kutoka matopeni na mavumbini.

Katika nchi yetu wapo wale wanaokemea uovu, wanaotukumbusha kwamba tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, si sura na mfano wa shetani.

Wapo watakatifu katika jamii yetu, ambao wanasikia mayowe, vilio na mateso ya wale wanaonewa na kuteswa, wale ambao ni kimbilio la wanyonge, ambao wapo tayari kukemea uovu po pote walipo.

Ni watu wa aina hii kati yetu wanatuhakikishia kwamba hatukuumbwa tuwe na mioyo baridi, tuwe wachoyo na wabinafsi, la hasha. Hatukuumbwa tuwe hatari kwa wenzetu, bali tuwe kimbilio la wanyonge na wenye tabu.

Ni watu wa aina hii wanatufanya sisi wote tuwe na tumaini kwamba kesho yetu itakuwa bora kuliko leo na jana, na kwamba kweli ubinadamu na utu wetu una maana pale mioyo yetu inapojaa joto la upendo, ukarimu na heshima kwa wengine.

Kama vile binadamu anaweza kuwa mtu hatari sana kwa wengine, anaweza pia kuwa baraka na neema kwa wengine.

Huu ndio mtihani wa msingi kuliko yote katika ubinadamu wetu. Hivyo nimezidi kuamini kwamba utu wetu na ubinadamu wetu una maana pale tunapoishi kwa upendo, ukarimu, na kuwajali wengine, hasa wanaoteseka, wanaogandamizwa na wahitaji.

 Ndiyo maana Mhubiri TB Joshua anasema: mikono yako yaweza kujaa fedha, akili yako yaweza kujaa maarifa na elimu, lakini kama moyo wako haukujaa joto la upendo, maisha yako si chochote.

Hili ndilo somo lipitalo masomo yote, ndilo somo la falsafa zote, ndilo somo linalofundishwa na misahafu yote, ndilo somo kuu la makala haya ya leo.