Rasmi Samatta kuicheza Le Havre Ufaransa

Nyota wa soka wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta, amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuichezea Le Havre inayoshiriki Ligi Kuu Ufaransa (Ligue 1), hatua inayoweka historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza Mtanzania kucheza katika ligi hiyo ya juu  nchini humo.

Le Havre wamemtambulisha mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 32, wakithibitisha kuwa atavaa jezi namba 70 katika timu hiyo inayofahamika kama Sky & Navy. Uhamisho huo unakuja baada ya Samatta kuwa na mafanikio makubwa akianzia Afrika hadi kwenye baadhi ya ligi za Ulaya.

Kwa mujibu wa tovuti rasmi ya klabu hiyo, Samatta amesajiliwa kutokana na uzoefu, ubora wa kiufundi pamoja na uwezo wa kumalizia kwa ustadi.

“Nchini Tanzania, kuna hazina mbili kubwa zisizopingika: Mlima Kilimanjaro na Ally Samatta. Na wakati Le Havre si wageni wa kupanda milima mirefu, safari hii wameamua kuleta mlima wa vipaji moja kwa moja Normandy,” ilisomeka taarifa kwenye tovuti ya klabu.

Akiwa na jina la utani Samagoal kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufumania nyavu, Samatta alijizolea umaarufu akiwa na TP Mazembe ya DR Congo ambako alishinda mataji manne ya ligi na kuisaidia timu hiyo kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika 2015.

Katika mwaka huohuo, alimaliza akiwa mfungaji bora wa mashindano hayo na kutangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Afrika anayecheza barani humo.

Ufanisi wake Afrika ulimfungulia milango Ulaya akiianza safari yake katika timu ya Genk ya Ubelgiji na akiwa huko aliisaidia kutwaa taji la Ligi Kuu Ubelgiji na kujitokeza kuwa mmoja wa washambuliaji tishio zaidi katika ligi hiyo.

Uwezo wake ulimpa nafasi ya kujiunga na Aston Villa ya Ligi Kuu England kisha akacheza Fenerbahçe (Uturuki), Royal Antwerp (Ubelgiji) na kurejea kwa mara ya pili Genk.

Hivi karibuni, Samatta alikuwa akiitumikia PAOK Thessaloniki ya Ugiriki, ambako alicheza nafasi muhimu katika kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Super League 2023–24.

Akiwa na Le Havre, Samatta anarajiwa kuleta si tu uzoefu, bali pia uwezo wa kuamua matokeo katika mechi.