Saba kortini wakidaiwa kuingiza tani 11 za dawa za kulevya

Dar es Salaam. Washtakiwa saba, wakiwemo raia wa Sri Lanka wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka moja la kuingiza sampuli za dawa za kulevya aina ya mitragyna speciosa zenye uzito wa kilo 11,596.

Dawa hizo zinaelezwa kuwa na madhara sawa na heroini, kokeini na methamphetamine. Miongoni mwa madhara yake kwa watumiaji ni kupoteza kumbukumbu.

Wakili wa Serikali, Eric Davies, leo Agosti 5, 2025  amewataja washtakiwa hao kuwa ni Riziki Shaweji (40) mfanyabiashara na mkazi wa Masaki, Andrew Nyembe (34) wakala wa forodha,  Mariam Ngatila (40) mfanyabiashara na mkazi wa Masaki na Ramadhani Said (57) mfanyabiashara mkazi wa Kifuru.

Wengine ni dereva, Godwin Maffikiri (40) mkazi wa Oysterbay na wafanyabiashara wawili raia wa Sri Lanka, Jagath Wellalage (46) mkazi wa Kinondoni na Santhush Hewage (25) mkazi wa Masaki.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga amedai washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ya mwaka 2025.

Amedai washtakiwa wanadaiwa Julai Mosi, 2025 katika bandari kavu ya Said Salim Bakhresa (SSB- ICD) iliyopo eneo la Sokota wilayani Temeke, kwa pamoja waliingiza sampuli zenye uhusiano na dawa za kulevya aina ya mitragyna speciosa zenye uzito wa kilo 11,596 (sawa na tani 11.5).

Wanadaiwa kuingiza dawa hizo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume cha sheria.

Wakili Davies amedai shtaka hilo halina dhamana kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, inayoeleza ikiwa dawa za kulevya za aina hiyo zinazidi kilo 30, kesi inakuwa haina dhamana.

Hakimu Kiswaga amesema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi. Pia shtaka linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Amesema tarehe ijayo kesi itatajwa kwa njia ya video, hivyo aliiahirisha hadi Agosti 19, 2025 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamepelekwa rumande.