MICHUANO ya fainali za Kombe la Ubingwa kwa Nchi za Afrika (CHAN) 2024 inaendelea tena leo kwa mechi mbili za Kundi D zitakazopigwa visiwani Zanzibar, lakini macho na masikio yanaelekezwa katika pambano la watetezi, Senegal ‘Simba wa Teranga’ dhidi ya Super Eagles ya Nigeria.
Pambano hilo litakalopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex kuanzia saa 2:00 usiku, litatanguliwa na mechi ya mapema saa 11:00 jioni kati ya Congo Brazzaville dhidi ya Sudan.
Senegal inashiriki michuano hii kwa mara ya tatu baada ya kufanya hivyo 2011 na 2022 ilipotwaa taji hilo katika fainali dhidi ya Algeria kwa penalti 5-4 na miamba hiyo kutoka suluhu (0-0) dakika 120.
Kikosi hicho kinachoshika nafasi ya 18 katika viwango vya ubora wa FIFA, kikifundishwa na kocha Souleymane Diallo, kilipata tiketi ya kushiriki CHAN 2024 kwa kuitoa Liberia kwa jumla ya mabao 4-1.
Kwa upande wa Nigeria, inashiriki michuano ya CHAN kwa nne kuanzia 2014, 2016, 2018 na 2024 na kwa ubora wa viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) zilizotolewa Julai 2025, kikosi hicho cha Super Eagles, kiko nafasi ya 43.
Nigeria inayonolewa na Kocha Daniel Ogunmodede, ilikata tiketi ya kushiriki CHAN 2024 baada ya kuitoa Ghana kwa jumla ya mabao 3-1, huku nahodha na nyota wa kikosi hicho, Junior Nduka akionyesha kiwango bora katika mechi hiyo.
Ushiriki bora wa CHAN ni wa 2018, ilipofika fainali na kukosa ubingwa mbele ya wenyeji Morocco, baada ya kuchapwa 4-0, yaliyofungwa na Zakaria Hadraf aliyefunga mawili, huku Walid El Karti na Ayoub El Kaabi wakifunga moja moja.
Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana, ilikuwa ni mechi ya kirafiki na Senegal ilishinda bao 1-0 katika pambano la kuvutia lililopigwa, Juni 16, 2019, huku mechi ya aina hiyo iliyopigwa Machi 23, 2017, zilitoka sare ya kufungana bao 1-1.
Katika mechi nyingine ya saa 11:00 jioni, Congo ‘The Red Devils’, inashiriki michuano hii kwa mara ya tano baa da ya 2014, 2018, 2020 na 2022, huku katika ubora wa viwango vya FIFA Duniani, kikosi hicho kinashika nafasi ya 132.
Kiwango bora cha timu hiyo katika michuano ya CHAN ni kuishia hatua ya robo fainali, ikianza mwaka 2018 na kupoteza kwa penalti 5-3, dhidi ya Libya, baada ya miamba hiyo kutoka sare ya kufungana bao 1-1, kutokana na mechi hiyo kuchezwa dakika 120.
Robo fainali nyingine kufika ilikuwa ni ya 2020 katika fainali zilizofanyika Cameroon na kikosi hicho pia kiliendelea mkosi wa kutolewa tena kwa penalti 5-4, dhidi ya Mali, baada ya pambano hilo kuisha kwa suluhu (0-0), dakika 120.
Kwa upande wa Sudan ‘Falcons of Jediane’, inashiriki michuano hii kwa mara ya tatu tu baada ya kufanya hivyo mwaka 2011 ikiwa wenyeji na 2022 iliposhiriki tena Algeria, huku kikosi hicho kikishika nafasi ya 113 kwa ubora wa viwango vya FIFA.
Kiwango bora cha kikosi hicho kwenye michuano ya CHAN, ni kumaliza mshindi wa tatu mwaka 2011 ikiwa mwenyeji, baada ya kuifunga Algeria bao 1-0, lililofungwa na Mudather Karika dakika ya 37, katika pambano lililopigwa Februari 25, 2011.
Sudan ilifuzu CHAN kwa kucheza raundi mbili, ikianza ya kwanza kwa kuifunga Tanzania bao 1-0, kisha mechi ya marudiano ikachapwa pia 1-0, huku hatua ya pili ikaitoa Ethiopia kwa jumla ya 2-1, ikianza kwa kushinda 2-0 na kuchapwa ugenini 1-0.
Kocha Kwesi Appiah raia wa Ghana ndiye anayekiongoza kikosi hicho katika michuano ya CHAN 2024, akichukua nafasi ya Mmorocco Badou Zaki, aliyeondoka baada ya kushindwa kufuzu mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) Ivory Coast 2023.
Appiah amefundisha klabu mbalimbali zikiwemo, Asante Kotoko ya kwao Ghana na Al Khartoum ya Sudan kati ya mwaka 2014 na 2017, huku akifundisha pia timu ya Taifa ya Ghana kuanzia 2012 hadi 2014, akiwa amezaliwa Juni 30, 1960, huko Kumasi.