TIMU za taifa za Sudan ‘Falcons of Jediane’ na Congo zimeshindwa kutambiana katika mechi ya kwanza ya kundi D ya michuano ya Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, Sudan ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 29, kupitia kwa nyota wa kikosi hicho, Musa Hussein Musa, baada ya kuwazidi ujanja safu ya mabeki ya Congo.
Pambano hilo la kuvutia kwa timu zote mbili, lilishuhudia Congo ikisawazisha bao hilo dakika ya 86 kupitia kwa Carly Ekongo Landou na kuzifanya timu hizo kugawana pointi moja katika mechi hiyo ya kwanza ya kundi D.
Congo ‘The Red Devils’, inashiriki CHAN kwa mara ya tano, baada ya kufanya hivyo mwaka 2014, 2018, 2020, 2022 na 2024, huku kiwango bora katika michuano hiyo ni kuishia hatua ya robo fainali mara zote mbili.
Congo inayonolewa na Kocha Mkuu,
Barthelemy Ngatsono, iilianza kutolewa robo fainali ya mwaka 2018, kwa kupoteza kwa penalti 5-3, dhidi ya Libya, baada ya sare ya bao 1-1, kufuatia mechi hiyo kuchezwa dakika 120.
Robo fainali nyingine kufika, ilikuwa ni ya mwaka 2020, katika fainali hizo zilizofanyika Cameroon, ambapo kikosi hicho pia kiliendelea mkosi wa kutolewa tena kwa penalti 5-4, dhidi ya Mali, baada ya pambano hilo kuisha kwa suluhu (0-0), ndani ya dakika 120.
Kwa upande wa Sudan inayonolewa na Mghana Kwesi Appiah aliyerithi nafasi ya Mmorocco Badou Zaki, inashiriki michuano hii kwa mara ya tatu baada ya mwaka 2011, ilipokuwa wenyeji na 2022 iliposhiriki tena fainali za Algeria.
Kiwango bora cha kikosi hicho kwenye michuano ya CHAN, ni kumaliza mshindi wa tatu mwaka 2011 ikiwa ndio mwenyeji, baada ya kuifunga Algeria bao 1-0, lililofungwa na Mudather Karika dakika ya 37, katika pambano lililopigwa Februari 25, 2011.
Sudan ilifuzu CHAN kwa kucheza raundi mbili, ikianza ya kwanza kwa kuifunga Tanzania bao 1-0, kisha mechi ya marudiano ikachapwa pia 1-0, huku hatua ya pili ikaitoa Ethiopia kwa jumla ya 2-1, ikianza kwa kushinda 2-0 na kuchapwa ugenini 1-0.
Matokeo haya yanazifanya timu hizi kugawana pointi moja kabla ya kusuhiri pambano lingine la saa 2:00 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar, litakaloshuhudia mabingwa watetezi Senegal ikivaana na Nigeria.