TAASISI YA NGUVU YA ATOMIC TANZANIA KUBORESHA UZALISHAJI WA KILIMO ‎


:::::::

 Na Ester Maile Dodoma 

‎Katika juhudi za kuboresha uzalishaji wa kilimo na kupambana na changamoto za njaa, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo Zanzibar kwa kushirikiana na Taasisi ya Nguvu ya Atomic Tanzania (TAEC) wameanzisha mradi wa kuzalisha mbegu bora za mpunga, zilizoboreshwa kwa kutumia mionzi ya nyuklia, zinazoongeza mavuno kwa kiasi kikubwa katika maeneo ya kilimo cha mpunga.

‎Akizungumza na waandishi wa habari, Hatibu Haji, mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar, alieleza kwamba mbegu hizi bora zimeweza kuongeza mavuno kutoka tani 7 hadi 9 kwa hekta moja, akitumia teknolojia ya mionzi ya Atomic Super Biss, ambayo ina uwezo wa kupambana na magonjwa mbalimbali ya mpunga. “Mbegu za Zaricc 3 na Zaricc 5 ambazo tumekuza zinatumika sana katika maeneo ya Zanzibar, na tumeweza kupata mafanikio makubwa kwa kupambana na magonjwa hatari ya mpunga,” alisema Haji.

‎Mbegu za Zaricc 3 zimetengenezwa ili kupambana na ugonjwa wa “Yellow Mottle Virus” (YMV), ugonjwa maarufu wa mpunga, huku mbegu za Zaricc 5 zikilenga kupambana na magonjwa ya mabakamabaka. “Hizi mbegu zinazoendelea kutumika kwa mafanikio katika maeneo ya Zanzibar, ni uthibitisho wa uwezo wa mionzi ya nyuklia katika kuboresha uzalishaji wa kilimo,” aliongeza Haji.

‎Vilevile, Haji alisisitiza kuwa mbegu hizi za nyuklia ni salama kwa matumizi ya binadamu, na kwamba wakulima wanapaswa kuzitumia kwa uhuru, kwani ni mbegu ambazo zimepata majaribio ya kina na kuonyesha uwezo mkubwa katika kutoa mavuno bora bila kuathiri afya ya walaji.

‎Naye, Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Nguvu ya Atomic Tanzania, Vitus Balobegwa, alielezea kuwa kauli mbiu ya mwaka huu ya maonesho ya Nanenane ni “ATOM KWA CHAKULA”, ikiwa na lengo la kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya nyuklia ili kuongeza usalama wa chakula na kuboresha uzalishaji katika kilimo.

‎”Teknolojia ya nyuklia ina matumizi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na matumizi ya nishati, kilimo, viwanda na hata sekta ya afya. Katika kilimo, tunatumia teknolojia hii kutengeneza mbegu bora, ambazo zinahimili changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi, na kuongeza mavuno,” alisema Balobegwa.

‎Balobegwa pia alielezea kuwa, mbinu za nyuklia katika kilimo zina uwezo wa kuongeza muda wa maisha ya mazao kwa kupunguza haraka kwao. “Mfano mzuri ni nyanya, ambapo tunatumia teknolojia ya nyuklia kuziangaza, na hivyo kuongeza muda wa kuishi na kupunguza upotevu wa chakula,” aliongeza.

Afisa Tehama kutoka Taasisi ya Nguvu ya Atomic Tanzania, Fadhili Msumali, alisema kuwa taasisi hiyo ina jukumu la kuhakikisha usalama wa vyanzo vyote vya mionzi nchini, na kuhimiza matumizi salama ya mionzi katika sekta ya kilimo na chakula. “TAEC inatoa leseni kwa watu wanaoshughulika na mionzi na bidhaa za chakula, mbolea na tumbaku, na tunatoa huduma kupitia mifumo ya mtandao kwa urahisi zaidi,” alisema Msumali.

‎Kwa kutumia mfumo wa mtandao wa Poto.Taec.go.Tz, wateja wanaweza kuomba vibali na leseni kwa urahisi, pamoja na kutuma sampuli kwa ajili ya vipimo kwenye ofisi za TAEC zilizopo katika maeneo ya mipakani na nchi nzima.

‎Taasisi ya Nguvu ya Atomic Tanzania inahakikisha kuwa teknolojia inayotumika ni salama na inaendelea kufuata taratibu na sheria zinazohusiana na usimamizi wa mionzi, ili kuhakikisha kwamba haitoi madhara kwa afya ya binadamu. Hii inahakikisha kuwa wakulima wanaweza kutumia teknolojia hii kwa manufaa ya kilimo bila wasiwasi wowote.

‎Kwa ujumla, juhudi hizi za kuboresha uzalishaji wa kilimo kwa kutumia mionzi ya nyuklia, sio tu kwamba zitasaidia kuongeza mavuno, bali pia zitachangia kupunguza njaa na kuongeza usalama wa chakula, hasa katika maeneo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.