KIPIGO cha mabao 3-0 ilichopewa Uganda The Cranes kutoka kwa Algeria katika mechi ya kwanza ya Fainali za CHAN 2024 jana usiku imeifanya timu hiyo kuingia anga za Ivory Coast.
Ivory Coast ikiwa wenyeji wa fainali za kwanza za CHAN 2009 ilikumbana na kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Zambia yaliyofungwa na Given Singuluma akiwa mchezaji pekee kufunga hat trick mechi za ufunguzi wa michuano hiyo hadi sasa.
Baada ya hapo, hakuna timu mwenyeji iliyopoteza mechi ya kwanza ya fainali hizo hadi jana usiku jijini Kampala ilipofumuliwa na Mbweha wa Atlas.
Uganda ni kati ya nchi tatu wenyeji wa fainali za 2024 ikiwamo Tanzania na Kenya ambazo zilianza mechi zao kwa ushindi zikifuata wenyeji wa fainali sita zilizopita zilizoanza na ushindi.
Sudan iliyokuwa wenyeji wa fainali za mwaka 2011, Afrika Kusini iliyoandaa 2014, Rwanda (2016), Morocco (2018), Cameroon (2020) na zile za mwaka 2022 zilizofanyika Algeria, kila moja ikianza na ushindi kama ilivyofanya Tanzania ilipoifunga Burkina Faso kwa mabao 2-0 na Kenya iliyoinyoa DR Congo bao 1-0.
Sudan ilianza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Gabon, Afrika Kusini iliichapa Msumbiji kwa mabao 3-1, wakati Rwanda ilianza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ivory Coast mwaka 2016.
2018 wenyeji Morocco ilishinda mabao 4-0 mbele ya Mauritania, wakati Cameroon ianza na ushindi wa 1-0 mbele ya Zimbabwe na fainali zilizopita Algeria iliifumua Libya kwa bao 1-0.
Fainali za mwaka huu zilizoanza Agosti 2 zitafikia tamati Agosti 30 ikishirikisha nchi 19 na hadi jana usiku jumla ya mabao tisa yameshafungwa katika mechi sita, huku penalti ikiwa moja iliyopigwa na Abdul Suleiman ‘Sopu’ wa Tanzania na mechi moja pekee kati ya Madagascar na Mauritania ndiyo haikuzalisha bao lolote.