UMMY MWALIMU AFANIKIWA KUTETEA KITI CHAKE KUPITIA KURA ZA MAONI TANGA MJINI


 :::::::

Na: Mwandishi Wetu, Tanga

Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini aliyemaliza muda wake ambaye pia alikuwa akitetea nafasi yake kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ummy Mwalimu ameibuka mshindi katika mchakato wa kura za maoni ndani ya Chama chake kwa kupata jumla ya kura 5750 sawa na asilimia 56.

Ushindi huu wa kura za maoni dhidi ya wenzake wanne, unamfanya Ummy Mwalimu kusubiri baraka za Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ili kuthibitishwa. 

Kimsingi, endapo Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu itamthibitisha kuwa mgombea, basi Ummy Mwalimu atachuana na wagombea wengine kutoka vyama vya upinzani katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Tangu mwanzo, nyota ya Ummy Mwalimu ilionekana kung’ara kutokana na Wajumbe kutambua kazi nzuri alizozifanya katika kipindi cha uongozi wake ambapo miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa katika sekta za elimu, afya, maji, miundombinu, masoko, uvuvi, mifugo, viwanda, ajira na uwezeshaji wananchi kiuchumi. 

Ummy Mwalimu amekuwa Mbunge wa mfano katika Jimbo la Tanga Mjini ambapo katika kipindi kifupi cha miaka mitano akiwa Mbunge kamili wa Jimbo la Tanga Mjini, kasi ya maendeleo imekuwa kubwa.

Ikumbukwe, Ummy Mwalimu ni Mbunge wa kwanza mwanamke katika Jimbo la Tanga Mjini ambaye amethibitisha pasi na shaka uwezo mkubwa wa uongozi walionao wanawake. Katika hatua nyingine, Ummy Mwalimu amewashukuru Wajumbe kwa kumwamini huku akiahidi kuendelea kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Tanga Mjini kwa kuhakikisha kero zao zinapatiwa ufumbuzi.