10 wafanyiwa tiba ya teknolojia mpya JKCI

Dar es Salaam. Wagonjwa 10 wenye matatizo ya mapigo ya moyo yajulikanayo kitaalamu kama ‘heart rhythm disorders’ wamefanyiwa upasuaji wa moyo kupitia tundu dogo wakati wa kambi maalumu iliyofanyika kwa siku tano.

Awali matibabu hayo yalitolewa kupitia upasuaji mkubwa wa kufungua kifua.

Kambi hiyo maalumu imefanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Madaktari Africa la nchini Marekani na kumalizika hivi karibuni.

Lengo la kambi hiyo lilikuwa kuwasaidia wagonjwa pamoja na kuimarisha ujuzi wa teknolojia hiyo mpya kwa madaktari wa JKCI na kuwapa nafasi wanafunzi wa shahada ya udaktari kupata fursa ya kujifunza kwa vitendo.

Akizungumza leo Agosti 6, 2025 Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo JKCI, Yona Gandye amesema wagonjwa waliopatiwa matibabu katika kambi hiyo ni wale wenye matatizo katika mfumo wa utengenezaji wa mapigo ya moyo.

Amesema hali husababisha moyo kwenda kasi kupita kawaida, kuzimia na kuwa katika hatari ya kupoteza maisha.


“Kwa wakati huu tulikuwa tumeandaa wagonjwa zaidi ya 10 wenye hitilafu katika mfumo wa mapigo ya moyo ili waweze kufanyiwa upasuaji katika kambi hii, tatizo la mfumo wa mapigo ya moyo husababisha moyo kwenda kasi sana na unaweza kusababisha kifo cha ghafla,” amesema Dk Gandye.

Dk Gandye ameeleza kuwa wagonjwa wengi hawakuwa na uwezo wa kifedha, kulipia gharama za matibabu yao lakini JKCI kwa kushirikiana na Madaktari Africa walitoa huduma hizo bila kujali hali yao ya kifedha.

“Karibu asilimia 50 ya wagonjwa waliotibiwa safari hii hawakuwa na uwezo wa kulipia gharama za matibabu, lakini walipata huduma kupitia msaada wa JKCI na wa Madaktari Africa,” ameongeza Dk Gandye.

Kwa upande wake, Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo kutoka Shirika la Madaktari Africa, Matthew Sackett ameeleza kuwa wanapenda kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo ili kwa pamoja waweze kushirikiana na wataalamu wa JKCI katika kuokoa maisha na kuendeleza ujuzi wa ndani kwa wataalamu wa JKCI.

“Tumekuja na timu yetu kutoa huduma kwa wagonjwa pamoja na kutoa mafunzo ya kina kwa wataalamu wa JKCI kuhusu matibabu ya magonjwa ya mapigo ya moyo, ushirikiano wetu na wataalamu wa taasisi hii ni wa kipekee,” amesema Dk Sackett.

Mfumo wa utengenezaji wa mapigo ya moyo, ni mfumo wa umeme wa ndani ya moyo unaohakikisha moyo unapiga kwa mpangilio sahihi ili kusukuma damu vizuri katika mwili mzima.

Mfumo huu unajulikana pia kama mfumo wa upitishaji wa msukumo wa umeme wa moyo (cardiac conduction system).

Umuhimu wa mfumo huu, husaidia kudhibiti kasi na mpangilio wa mapigo ya moyo.

Unahakikisha damu inasukumwa kwa ufanisi kwenda mapafuni na kwenye sehemu zote za mwili.

Ikiwa mfumo huu utapata hitilafu, mtu anaweza kuwa na matatizo ya moyo kama vile arrhythmia (mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida) na wakati mwingine huhitaji kifaa cha kusaidia kama pacemaker.