Siha. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa ameliagiza Jeshi la Polisi kuendelea kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha linashughulikia masuala ya jinai ikiwemo kukomesha matukio ya utekaji nchini.
Mbali na hilo, ameliagiza jeshi hilo kudhibiti madereva wazembe na vyombo vya moto vilivyo chini ya viwango ambavyo havistahili kuwa barabarani ili kupunguza matukio ya ajali.
Bashungwa ameyasema hayo leo, Agosti 6,2025 wakati wa ufunguzi wa jengo jipya la Kituo cha Polisi Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, lililogharimu zaidi ya Sh300 milioni.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa.
“Nitumie nafasi hii kulielekeza Jeshi la Polisi kuendelea kuzingatia maelekezo mbalimbali yanayohusu masuala ya jinai ikiwemo kukomesha matukio ya utekaji, pamoja na kudhibiti madereva wazembe na vyombo vya moto vilivyo chini ya viwango ambavyo havistahili kuwa barabarani ili kupunguza ajali,”amesema Bashungwa
Aidha, amelitaka Jeshi hilo kuendelea kuharakisha upelelezi wa mashauri mbalimbali kwa kushirikiana na vyombo vingine vya haki jinai, na kuhakikisha linaboresha utoaji huduma kwa wananchi wanapofika katika vituo vya polisi nchini.
Pamoja na mambo mengine, amelitaka Jeshi hilo kuhakikisha linakomesha vitendo vya uvunjifu wa amani na uhalifu nchini na kuhakikisha tunu ya amani inakuwepo.

“Niwatie moyo msimuonee muhali mtu yeyote ambaye anaweza kutumika na watu wasioitendea mema nchi yetu kutumia kipindi hiki cha uchaguzi kuvuruga amani ya nchi yetu, vyombo vyote mshirikiane muungane kuhakikisha wahalifu wa namna hii wanatafuta kwenda mbali kabisa na Tanzania, yaani waione Tanzania sio nchi ya kuchezea,”amesema Bashungwa
Bashungwa, amelitaka Jeshi hilo kubainisha viongozi wa vituo vyote vya bodaboda nchini na kukaa nao ili kuona namna bora ya kuwapa elimu ili kuendelea kufuata sheria za usalama barabarani na kupunguza matukio ya ajali.
“Tubainishe viongozi wa vituo hivi vya bodaboda maeneo yote ya nchi na kukaa nao kuona namna ya kuwapa elimu kuendelea kuelimisha, kufuatilia na kuhimiza sheria za usalama barabarani ili mkakati huu uwe ni sehemu ya kukabiliana na changamoto za ajali barabarani,”amesema Bashungwa na kuongeza
“Wananchi tuwaombe ushirikiano, ukiwa ni abiria kwenye basi au chombo chochote cha usafiri ukaona dereva hawajibiki katika taaluma yake ya kuwa salama katika kuendesha kile chombo kuna namba za kupiga Jeshi la Polisi.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini a(IGP), Cammilius Wambura amesema mpaka sasa nchi ni salama na hakuna uvunjifu wowote wa amani.

“Nchi yetu ni salama mpaka hapa tulipo na ni salama sana na hili naweza kuliongea sehemu yoyote ni ndani ya nchi au nje ya nchi kama Mkuu wa Jeshi la Polisi, nina ongea kwamba nchi yetu ni salama na itaendelea kuwa salama,”amesema Wambura
Aidha amewataka Watanzania kushirikiana na Jeshi hilo kuhakikisha amani, utulivu na usalama wa nchi unakuwepo.
“Asitokee mtu yeyote popote pale atokapo akawadanganya, msikubaki kudanganyika, thamani ya usalama wetu ni kubwa kuliko chochote lakini naomba nitumie jukwaa hili niwakumbushe Watanzania kwamba kuvuruga amani ya nchi ni suala la dakika moja, kurudisha amani ya nchi gharama yake ni kubwa sana,”amesema IGP Wambura.
Amesema, “hapa ndio nyumbani kwetu hatuna sehemu nyingine ya kwenda kuishi na ninaamini wengi tulikuwa tukishuhudia wananchi wakitafuta sehemu salama za nchi.”
Pamoja na mambo mengine, amewapongeza wananchi wa wilaya ya Siha kwa kushirikiana na Jeshi hilo kuhakikisha ujenzi wa kituo hicho cha polisi kinakamilika.
“Niwapongeze wananchi wa Wilaya ya Siha kwa moyo wao wa uzalendo na kujitolea kuhakikisha ujenzi wa kituo hiki unakamilika, Serikali ilitoa Sh318 milioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu na wananchi kwa upande wao wamechangia Sh179 milioni,”amesema IGP Wambura
Naye, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema katika mkoa huo kuna uhitaji mkubwa wa nyumba za askari hali inayosababisha wengi wao kuishi uraiani, jambo ambalo linaathiri utendaji kazi wao.