ELIMU YA UBORA WA BIDHAA YAONGEZA HAMASA KWA WAJASIRIAMALI WA KANDA YA KASKAZINI

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limewataka Wajasiriamali kutoka halmashauri 21 za mikoa ya Kanda ya Kaskazini kuthibitisha ubora wa bidhaa zao ili kuweza kupata masoko ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na soko huru la biashara ukanda wa Afrika.

Wito huo umetolewa leo Agosti 6, 2025 katika Viwanja vya Themi Njiro Jijini Arusha kwenye maonesho ya wakulima ya Nane Nane na Meneja wa TBS Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Joseph Ismail wakati wa utoaji elimu kwa wajasirimali na wafanyabiashara ili waweze kushindana sokoni na kujikwamua kiuchumi.

Amesema TBS kupitia maonesho hayo ya kilimo yenye kauli mbiu ya Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025,ambapo wanawatembelea wajasiriamali waliopo katika halmashauri zote 21 ili kutoa elimu na kupata kanzi data yao ili waweze kupata alama za ubora wa bidhaa kutoka TBS.

“Tunazunguka halmashauri zote za Kanda ya Kaskazini zilizopo hapa kwalengo la kutoa elimu ili kuhakikisha bidhaa wanazozalisha zinakuwa na alama za ubora ili kuweza kuuzwa ndani na nje ya nchi ikiwemo soko huru ukanda wa Afrika” amesema.

Aidha amesema katika maonesho hayo TBS wanatoa elimu zaidi kwao ili waweze kupata alama na kuweza kushindana katika masoko ya ndani ,EAC na soko huru la Afrika ambalo wafanyabishara wanalipambania ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Amesisitiza TBS kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabishara na wajasirimali ili kuhakikisha wanapata fursa za bidhaa zao kuuzwa kwa kuwa na nembo za ubora kwani wajasiriamali hao hawapaswi kuwa wafanyabishara wadogo pekee lazima wawe na vigezo vya utambulisho wa ubora wa bidhaa zao.

Nao baadhi ya wajasiriamali hao kutoka halmashauri ya Karatu, Ngorongoro ambao ni Adili Msangi anayetengeza mbolea yenye mchanganyiko wa mkojo wa ng’ombe na molasisi na Marta Kamili anayetengeza asali kutoka halmashauri ya Karatu na Elizabeth John kutoka Ngorongoro walishukuru kupata elimu hiyo na watahakikisha bidhaa zao zinathibitishwa na kuingia sokoni na kushindana huru ndani na nje ya nchi.