Familia ya mtia nia aliyetoweka yaibua mapya

Tarime. Ikiwa leo ni siku ya tisa tangu mtiania wa udiwani katika kata ya Ganyange wilayani Tarime, Siza Mwita na rafiki yake, Anthony Gabriel kutoweka katika mazingira ya kutatanisha, familia imetuma ujumbe wa watu watatu kwenda makao makuu ya Jeshi la Polisi ili kujua mustakabali wa ndugu zao.

Kwa upande wa kura za maoni zilizofanyika Agosti 4,2025 Siza alishika namba tatu kwa kupata kura 120 huku akizidiwa kura 22 na mshindi wa kwanza katika kinyang’anyiro hicho, licha ya kutoshiriki kwenye mchakato wa kura hizo za maoni ikiwa ni pamoja na kutokufanya kampeni.

Ujumbe huo wa watu watatu umeondoka wilayani Tarime mkoani Mara jana Agosti 5, 2025 ukiongozwa na mama mzazi wa Siza, Suzana Kehata.

Mtiania wa udiwani katika kata ya Ganyange wilayani Tarime, Siza Mwita (kushoto) akiwa na rafiki yake, Anthony Gabriel.



Siza na Anthony wote wakiwa ni wafanyabiashara wa usafirishaji, wanadaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha wakiwa safarini.

Gari lao lilipatikana likiwa limetelekezwa Nzega mjini mkoani Tabora.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora,  Richard Abwao amesema bado wanafanya uchunguzi wa tukio hilo kutokana na ukweli kuwa safari ya watu hao wawili, ilihusisha mikoa mbalimbali.

“Hii safari iko ‘connected’ na mikoa mbalimbali sio Tabora pekee, ndio maana tumeomba mtupatie muda kwa sababu tunafanya ufuatiliaji kwa kushirikiana na wenzangu wa mikoa hiyo, tukishapata taarifa kamili tutaitoa,” amesema Kamanda Abwao alipozungumza na Mwananchi.

Akizungumza na Mwananchi leo Agosti 6, 2025, Binamu wa Siza, Gabriel Kisogwe amedai familia imefikia hatua hiyo kwa lengo la kutaka kujua walipo ndugu zao baada ya Jeshi la Polisi kukaa kimya kwa muda wote tangu kupotea kwa ndugu zao.

“Watu wawili wamepotea, hawajulikani walipo leo ni siku karibia ya kumi mamlaka husika ipo kimya, kwa kweli inasikitisha sana,” amesema Kisogwe.

Amesema uamuzi wa familia wa kumtuma mama mzazi kufuatilia hatima ya ndugu zao, umetokana na ukweli kuwa hali ya mama inazidi kuwa mbaya kiasi kwamba, wameanza kuwa na hofu juu ya usalama wa maisha yake licha ya mama huyo kuonyesha kuwa yuko imara.

Mtiania wa udiwani Ganyange katika halmashauri ya wilaya ya Tarime ambaye pia ni mfanyabiashara wa usafirishaji, Siza Mwita anayedaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.



“Huyu mama ni mcha Mungu sana na anaishi maisha yake kama mama wa Kiafrika kabisa, muda wote anasema Mungu yupo na akina Siza watarejea salama, lakini ukimuangalia vizuri unabaini kuwa ana maumivu makali, yaani ameamua kuumia kimyakimya jambo ambalo sio zuri hata kiafya,” amesema.

Kisogwe amesema wanaamini mama huyo na ujumbe wake atakapofika makao makuu ya jeshi hilo watapata taarifa kamili na rasmi juu ya kile kinachoendelea kuhusiana na tukio la watu hao kutoweka baada ya kusubiri kwa siku tisa  bila kupata taarifa rasmi, kutoka jeshi hilo mkoani Tabora.

Kuhusu matokeo ya kura za maoni zilizopigwa Agosti 4, 2025, Kisogwe amesema Siza ameshika nafasi ya tatu huku akizidiwa kura 22 na mshindi wa kwanza.

Amesema anaamini endapo ndugu yao angepata nafasi ya kufanya kampeni, huenda angeongoza.

“Siza ni mtu wa watu, hebu fikiria hakuwepo kwa maana siku jina lake limerudishwa, ndiyo amepata matatizo haya, kwa hiyo hakushiriki kwenye kampeni na hakuwepo ndani ya kata yake na wilayani kwake lakini bado ameweza kupata kura hizo, sasa jiulize angeshiriki mchakato mzima angepata kura ngapi?,” amehoji.

Amesema katika uchaguzi huo kulikuwa na jumla ya wagombea wanne waliokuwa wakichuna kwenye kura hizo za maoni ambao ni John Gatende (142), Nashon (140), Siza Mwita (120) na Kennedy Mwikwabe (6). Licha ya kuwa mtiania wa udiwani, pia Siza alikuwa ni diwani wa kata hiyo ya Ganyange aliyemaliza muda wake.

Siza na mwenzake wanadaiwa kuondoka mjini Tarime Julai 29, 2025 kwenda safari ya kikazi, ghafla walipoteza mawasiliano na ndugu zao kabla ya gari lao kupatikana Nzega mjini mkoani Tabora.

Inadaiwa baada ya gari kupatikana likiwa limetelekezwa, baadhi ya ndugu wakiongozana na askari polisi walivunja vitasa vya gari na walikuta nguo zao.

Inadaiwa nguo hizo zilikuwa zimetolewa  kwenye mabegi huku baadhi ya vitu kama miswaki ikikutwa imedondoka chini kwenye gari hilo.