Kama huamini kama mimi, jua una matatizo makubwa na mengi. Tangu ishuke ‘neema’ kama manna, yaani uchakachuaji, kwa wenye meno na wanjanja, ni wakati wa kufyatua kwa mikono na miguu na kutanua au wa mboga saba japo si wote.
Wanene wapanue mikanda huku wadogo wakiifunga zaidi ili wanene wapate chakula na kutanua. Hadi hapa, nani haoni miujiza hii? Kama huoni wewe ni kipofu. Kama huifaidi, basi una laana, maana, hata chawa wanafaidi na kunenepeana.
Leo, nitazamia dhana ya kufyatua kwa mikono na miguu tena bila kunawa wala kuomba itokanayo na neema ya uchakachuaji. Unanawa nini wakati usafi na uchafu havina mpaka?
Unamwomba nani wakati ufyatuacho ni chako hata kama si chako? Utashindwaje kufyatua wakati una hamu na si njaa ya kula? Wasiofyatua na kukamua kama wewe wana ugonjwa wa akili au bulimia, yaani kuishiwa hamu ya kula. Nani anaweza kulala njaa wakati huu ambapo ulaji uko nje nje?
Huu ni wakati wa kumshukuru Mungu mkuu na miungu midogo na kushangilia neema japo nakama kwa wengine wasio na zana za kufyatulia katika dhana ya ufyatuaji tokana na matokeo yake.
Naona yule anatikisa kichwa! Huna haja ndugu yangu. Kama hushangilii hii neema, jua una roho mbaya kama Gen Z waliotaka kuchukua chakula cha wenyewe na kuwapa wote.
Nani kakwambia kuwa manna ni kwa dunia nzima? Manna ni kwa wana wateule wa mwenda usiku. Manna ni chakula cha wanjanja.
Kwa nini tusishangilie kwa kufufua miujiza na kuongeza mingine? Hakuna msimu mzuri kama huu wa uchakachuaji na ufyatuaji, sorry, uchaguzi. Unachagua kufyatua, kufyatuka, au kufyatuliwa hadi Novemba.
Nawashauri wasioshangilia wala kufaidi ufyatuaji huu wa manna wawe wavumilivu.
Hamjaambiwa? Mvumilivu hufyatua mbivu hata kama imeoza, Nani asiye na kisu aweza kula nyama? Ili ufyatue nyama, sorry, manna, wapaswa kuwa na kisu cha aina gani? Ni simpo.
Kisu hiki kinaitwa kura ya kula. Ukiwa na kisu hiki, unatoa ahadi ya kutoa kura ya kula kwa kila mtia nia halafu unaanza kufyatua kwa utulivu hata kama wapo watakaopiga makelele.
Hayo yasikutishe. Wahenga walisema. Kelele za chura hazizuii tembo kunywa maji. Nani anajali kelele za mpangaji wakati ni mwenye nyumba?
Ili kufyatua na kushangilia kwenye falsafa ya takrima, yakupasa uunganishe hata kwa kutenganisha.
Unawaunganisha maadui na kuwatenga na kupingana huku ukiwatosa wenye kupiga kelele. Unaunganisha matumbo badala ya sera. Kufyatua inageuka sera na sera inageuka ufyatuaji.
Si inapendeza siyo? Nani hataki kufyatua tena bila kutoa jasho? Hata aitwe kupe, msaliti na majina mengine mazuri, mfyatuaji ni mfyatuaji. Wahenga wanaasa. Mla kala leo, kesho kalani.
Isitoshe, cha mgema siku hizi, kinafyatuliwa na mlevi. Hamjaambiwa kwa umdhaniaye ndiye siye? Sasa inakuwaje awe ndiye wakati siye?
Haya ni maneno ya busara. Si mafumbo ili yahitaji mwelevu kuyang’amua.
Lazima tushangilie hata kusherehekea ufyatuaji maana, hata kama manna yenyewe ni wenzetu. Kwani, ni nyoka walao nyoka wenzao au samaki ama na waja wamejifunza sayansi hii ya ulaji?
Huko nitokako, kuna kamsemo kuwa mali ya umma haiumi hata uiume vipi. Kwani, wewe siyo umma? Hii ndiyo demokrasia, yaani, utawala wa watu kwa ajili ya watu. Uzuri wa demokrasia hii ya kukopa, haielezi watu ni wangapi.
Hata wawili ni watu. Haitofautishi uchakachuaji na uchaguzi. Hivyo, ni demokrasia. Nadhani tumeelewana. Sitaki maswali mengi. Yanini wakati huu ni wakati wa kula?
Nirejee falsafa ya takrima japo si ukarimu bali kuzidiana kete na kufyatuana kinamna. Mnaotaka kufyatua, mjue. Lazima mfyatuliwe na wale mtakaowafyatua baadaye kwa miaka mitano.
Hivyo, msipofyatua au kufyatuliwa, msilaumu wala kuumia. Ngoja tufyatue tushibe halafu tunapanue keki ya kaya ili wote mle. Kuna ufyatuaji aina mbili. Upo ule wa vitendo na ule wa imani. Nawashaurini muache malalamiko na ubishi.
Muishike imani ya kufyatua kwa imani si kwa vitendo ili msije kuvimbiwa mkakufuru. Hili ndilo sharti kuu la kula manna.
Najua. Wapo wabishi na wenye dhambi ya ubishi. Watahoji ni kwanini hawa wanakula na wale hawala au kuliwa. Wote tunakula.
Tunakula kwa kuwakilishana iwe ni kwa maeneo au vyama vyetu. Viongozi wakila, wanafanya hivyo kwa niaba ya waliowachagua ili wale. Kwa wenye ‘busara’ kula si jambo la kuwasumbua kwa vile wanaogopa kuvimbiwa wakakosa usingizi. Kwani, hamjui. Akosaye usingizi kwa kuvimbiwa na aukosaye kwa njaa wote wanaukosa. Kipi bora, kukosa usingizi wa kuvimbiwa au kutokula kabisa?
Ni suala la kutumia akili. Hivyo, wote tushangilie neema hii ya manna bila kujali nani anakula na nani anamla au kumlia mwenzake. Cha muhimu, msisahau kuongeza ulipaji kodi ili manna iongezeka ili tuibe, sorry, tuimbe, kushangilia na kufurahi. Muhimu tujue. Kila afyatuaye wengine, naye atafyatuliwa. Hivi niko wapi?