NYOTA wa riadha wa kimataifa wa Tanzania, Gabriel Geay atakuwa mzigoni tena na mara hii akitarajiwa kutimka katika mbio za Berlin Marathon nchini Ujerumani, Septemba 21, mwaka huu.
Katika mbio hizo mwanariadha huyo Mtanzania atakuwa sambamba na wanariadha kibao kutoka sehemu mbalimbali akiwamo Mkenya Sabastian Sawe mwenye umri wa miaka 30 ambaye kwa sasa anashikilia nafasi ya tano kwenye orodha ya muda bora duniani kwa upande wa mbio ndefu.
Sawe anarudi Berlin akiwa na matarajio makubwa baada ya kufanya vyema katika mbio zake mbili za kwanza za marathoni.
Mkenya huyo aliushangaza ulimwengu wa riadha baada ya kushinda Valencia Marathon, Desemba 2024 kwa muda wa 2:02:05, ukiwa muda wa pili bora zaidi kwa mwanariadha anayeanza kushiriki marathoni, kisha akatetea ubora wake kwa kushinda mbio za London Marathon ambazo zilifanyika Aprili, mwaka huu kwa muda wa 2:02:27.
Si mgeni jijini Berlin, Sawe alishawahi kushinda mbio za Berlin Half Marathon 2023, hatua iliyompa imani ya kurejea kwenye barabara hizo zenye historia ya rekodi za dunia.
Mkurugenzi wa mbio hizo, Mark Milde anaeleza furaha yake kurejea Sawe katika jiji hilo la Ujerumani.
“Tunafurahishwa na kutambuliwa kwa mbio za BMW Berlin Marathon na mwinuko wake usio na changamoto. Tayari Sawe alishawahi kuvutia Berlin aliposhinda nusu marathoni mwaka 2023. Bila shaka mwaka huu kutakuwa na ushindani mkali,” anasema.
Sawe anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa wanariadha mahiri akiwemo Milkesa Mengesha wa Ethiopia, bingwa mtetezi akitamba na muda wake bora binafsi 2:03:17 aliposhinda Berlin mwaka jana.
Yupo pia nyota wa kimataifa wa Tanzania, Geay mwenye muda bora wa saa 2:03:00 alioupata Valencia mwaka 2023.
Wote wawili ni wazoefu na wana kasi, lakini hali ya juu ya Sawe kwa sasa na kupanda kwa kasi kimataifa inamfanya kuwa kinara anayepewa nafasi kubwa kabla ya mbio kuanza.
Geay ambaye alikumbana na changamoto nyingi 2024 alionyesha dalili ya kurejea kwenye ubora wake kwa kushinda mashindano huko Daegu, Korea Kusini mapema mwaka huu kwa muda wa saa 2:05:20 jambo ambalo linawafanya Watanzania waamini katika mbio za Berlin kuwa ndiye atashinda.
Zaidi ya mafanikio yake kwenye marathoni kamili, Sawe pia ni bingwa wa dunia wa nusu marathoni – taji alilolichukua Riga 2023, jambo linalozidi kuthibitisha umahiri wake katika mashindano ya barabarani kwa umbali mbalimbali.
Kutokana na sifa ya Berlin kama njia ya haraka zaidi duniani kwa marathoni kuna uvumi unaoendelea kwamba Sawe anaweza kulenga kuvunja rekodi yake binafsi au hata ya dunia ambayo pia imevunjwa mjini humo katika miaka ya nyuma.
Barabara tambarare, miinuko ya chini na mazingira ya kasi endelevu huifanya Berlin kuwa eneo bora kwa maonyesho ya kihistoria.
“Hakuna mashindano mengine duniani yaliyoweka rekodi nyingi za dunia kama Berlin tangu 1998 kama waanzilishi wa Abbott World Marathon Majors tumeweka viwango vya juu”, anasema Jurgen Lock, mkurugenzi mtendaji wa waandaaji wa mbio hizo, SCC Events.
Mchanganyiko wa nguvu, ufanisi na maarifa ya mashindano ya Sawe unamfanya awe mshindani wa kipekee na huenda akawa tishio la rekodi ya dunia inayosubiriwa kuvunjwa.
Kama akifanikiwa, Sawe hatashinda tu mashindano mengine makubwa, bali ataandika jina lake katika historia ya marathoni ya dunia, lakini kwenye kutafuta rekodi yupo pia Geay ambaye anataka kushinda.
Mwaka huu ni shindano la 51 la Berlin Marathon – mashindano yanayojulikana kwa historia ya kuvunja rekodi, ambapo rekodi 13 za dunia zimewahi kuvunjwa kwenye njia zake tangu 1998.
Jiji hilo limekuwa sehemu ya mashindano ya heshima Abbott World Marathon Majors likiongoza kwa viwango vya juu vya kimataifa katika mchezo wa riadha. Hata hivyo kwa Geay hii ni fursa nyingine ya kuidhihirisha dunia kwamba Tanzania kuna miamba ya riadha inayotetea bendera ya nchi.