KOCHA mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge ameonyesha kuvutiwa na kiwango cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa stars’ katika mashindano ya CHAN baada ya kuifunga Burkina Faso kwa mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza.
Ibenge yupo wilayani Karatu mkoani Arusha, ambako timu yake iko kwenye kambi ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la Shirikisho Afrika.
Akichambua mchezo huo, alieleza kufurahishwa jinsi wachezaji walivyocheza akisema Tanzania ina uwezo mkubwa na inaweza kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.
Kocha huyo alionyesha kufurahiswa na muunganiko mzuri wa wachezaji, jambo ambalo linawapa nguvu na kuimarisha ushindani wao, hasa ukizingatia wanacheza nyumbani mbele ya mashabiki wao.
“Niliburudika kiukweli. Tanzania ni timu hatari katika haya mashindano. Wamefanya vizuri katika mchezo wa kwanza. Nawatakiwa kila la heri kwenye mchezo wao ujao,” alisema.
“Wanaweza kutwaa ubingwa kwa sababu, wanajuana vizuri, wanacheza kwa pamoja kitu kinachowafanya wawe na muunganiko mzuri. Pia wanacheza nyumbani na wana mashabiki wengi, nadhani watafanya vizuri na kutwaa ubingwa.”
Akizungumzia kiwango kilichoonyeshwa na nyota wa Azam katika mchezo huo, alisema walifanya vizuri – Sopu akifunga goli la kwanza na Nado alitoa pasi ya bao huku Feisal Salum alikuwa kwenye ubora wake.
Akizungumzia kambi ambayo wameweka Karatu, huku wachezaji wengine wakiwa timu ya taifa wakati huo wakitarajiwa kusafiri kwenda Kigali, Rwanda, Ibenge alisema Azam inataka kuwa timu kubwa na unapokuwa mkubwa siku zote wachezaji wako lazima watacheza timu za taifa.
“Binafsi nataka mashindano yajayo tuwe na wachezaji zaidi ya tisa katika timu ya taifa,” alisema.