January Makamba na mtego CCM, kuwa fursa ya wapinzani

Aprili 2019, aliyekuwa Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba, alifanya mahojiano na kituo cha Radio One, Dar es Salaam, na kueleza kuwa uongozi ni sawa na koti la kuazima, hivyo ukiwa kiongozi lazima uwe tayari kuishi bila koti pale mwenye nalo anapolichukua.

Alilenga kuwakumbusha wenye kushika uongozi, hasa vijana, kutojinyanyua na kuishi kwa mikogo, maana nafasi ambazo wanazishikilia si za kudumu. Wakati wowote watazipoteza halafu watashindwa kunyanyua nyuso kwa aibu.

January alisema kuwa yeye alikuwa akiwatazama vijana viongozi jinsi wanavyoziishi hadhi kubwa, wakitaka mpaka kufunguliwa mlango, wakibebewa mabegi yenye kompyuta zao za mpakato, wakati yote hayo wanaweza kujifanyia pasipo kupungukiwa kitu.

Wakati January akizungumza maneno hayo, alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Miezi mitatu baada ya January kuzungumza maneno hayo, Rais John Magufuli alitengua uwaziri wake.

Mpaka hapo ni rahisi ‘kubeti’ kuwa January alishajiandaa kuwa nje ya uwaziri. Alitambua kwamba cheo alichokuwa akishikilia siyo cha kudumu, maana ni koti la kuazima. Siku mwenyewe akilihitaji, hutakuwa na budi ya kuliacha.

Julai 29, 2025, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, alisoma kwa umma, orodha ya majina ya waliopitishwa na Kamati Kuu CCM, kwa ajili ya kuendelea kuwania uteuzi wa kuwa wagombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu 2025.

Katika orodha hiyo, January hakuwa mmoja wa waliopenya. Jina lake halikuvuka Kamati Kuu. Siku iliyofuata, Julai 30, 2025, alifuatwa na waandishi wa habari kwenye ofisi yake binafsi, Masaki, Dar es Salaam.

Swali la mwandishi: “Tunaomba kusikia neno lako, baada ya jina lako kukatwa jana na umepokeaje?”

January alijibu: “Kukatwa, hapana, kwanza kwenye CCM hii dhana ya kukatwa huwa haipo, ni aidha umependekezwa au hujateuliwa. Kukatwa maana yake kuna nafasi ambayo unaistahili na ni yako, kwa hiyo umekatwa.

“Wakati unapoomba nafasi hizi, wote mnakuwa mpo sawa. Hauistahili. Kama alivyowahi kusema Mwenezi wetu (Makalla), hakuna wazo la kukatwa, ni ama hukupendekezwa au hukuteuliwa. Kwa hiyo, sisi hatukuteuliwa, siyo kwamba tumekatwa.”

Akiendelea zaidi, January alisema, ndani ya CCM vikao ndiyo vina mamlaka ya maelekezo na uamuzi ambao unapaswa kuheshimiwa na wanachama pamoja na viongozi. Aliongeza kwamba yeye kama mwanachama mtiifu wa CCM amewajibika kupokea uamuzi.

Kuhusu kuridhika na uamuzi, January alisema, kuwa mwana-CCM maana yake ni kujifunga kwenye taratibu za chama, kwa hiyo uamuzi unapotolewa huna budi kupokea na kutoa saluti, kama ishara ya kuheshimu kilichoamuliwa.

January alikataa kuwa kuondolewa kwake inawezekana ni kumdhibiti mapema katika mbio zake za kuwania urais.

Alisema: “Kikao cha heshima kama Kamati Kuu, hakiwezi kufanya uamuzi kwa kutazama mambo ya mbeleni.”

Nimechukua matamshi hayo ya January ya nyakati mbili tofauti, ili kujenga mantiki kuhusu matokeo ya mchujo wa Kamati Kuu na uchaguzi wa ndani CCM, kupata wagombea ubunge na madiwani, vilevile historia ya vipindi kama hivyo.

Kwa miaka mingi, nyakati za mchakato wa kupata wagombea, CCM imekuwa ikiishi kwa presha kubwa. Hofu ambayo hutawala ni chama hicho kuwa fursa kwa vyama vingine, kupata wagombea wanaokubalika.

Tangu Uchaguzi Mkuu 1995, ambao ulikuwa wa kwanza wenye kushirikisha vyama vingi vya siasa tangu uhuru, CCM wamekuwa wakitengeneza wagombea wa vyama vya upinzani kila uchwao.

Kutoka Augustino Mrema hadi Edward Lowassa, nafasi ya urais, halafu Dk Willibrod Slaa mpaka John Shibuda, katika ubunge.

Ni utamaduni wa muda mrefu kuwa ukishindwa kupenya kwenye mchakato CCM, unaomba jukwaa upinzani, unagombea. Mrema na Lowassa, waliitikisa CCM katika urais. Slaa na Shibuda walishinda ubunge Chadema.

Si Slaa na Shibuda peke yake, majimbo mengi CCM iliyapoteza kutokana na mvurugano nyakati za uteuzi wa wagombea.

Wapo waliohamia upinzani na kushinda viti vya ubunge na udiwani. Wengine hawakushinda lakini waliathiri nguvu ya CCM, na kuacha upinzani ukibeba viti.

Presha ya kupoteza watu kwenda upinzani, kwa namna moja au nyingine, inaweza kuwa mtego kwa CCM, kupitisha wasiofaa kwa kuhofia wanaweza kwenda upinzani na kukisumbua chama chao.

Wajibu wa chama cha siasa, siyo kushinda dola peke yake, bali pia kuwapa wananchi mgombea sahihi. Presha za kupoteza kiti, zinaweza kufanya chama kimpitishe mtu asiye sahihi kwa sababu anaonekana kukubalika zaidi na watu.

Mapitio ya kauli ya January kuwa uongozi haumilikiwi na mtu, vilevile hakuna anayestahili uteuzi wa kuwa mgombea, bali vikao ndivyo vinaamua na uamuzi huo unapaswa kuheshimiwa, ni funzo la namna mwanachama na wataka uongozi jinsi wanapaswa kuwa.

Tabia ya watu kuhama vyama hovyo kufuata fursa za kugombea uongozi, ndiyo chanzo cha kuzalisha wanasiasa lukuki wasio na misingi. Mtu yupo kwenye chama fulani, hajui itikadi, desturi wala utamaduni wa taasisi aliyopo. Mradi aliona ni jukwaa la msako wa uongozi.

Mwanasiasa unapaswa kutambua kuwa uongozi unaombwa, kwa hiyo kuna kupewa au kunyimwa.

Ukipewa shukuru, na shukurani ni kwenda kuifanya kazi kwa uadilifu na moyo mkubwa. Ukinyimwa, unashukuru pia, kisha unasubiri wakati ujao.

Hulka ya kuomba uongozi kwa shinikizo la kufa au kupona, ndiyo hadithi ya mwanaisasa kugeuka mhamiaji wa vyama hata asivyovijua. Mwanasiasa anasimama jukwaani, anashindwa hata salamu ya chama anachotumia jukwaa lake. Katiba pia haijui. Mwisho, tunajenga nchi ya viongozi wajanja-wajanja.

Kauli ya January na mitazamo yake, haimpambanui tu kama kiongozi mwenye utulivu, anayejua azungumze nini na wakati gani, bali ni somo la wanasiasa kuheshimu michakato ya vyama. Hakuna mwenye hatimiliki ya uongozi.