Dar es Salaam. Aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amefariki dunia leo Jumatano, Agosti 6, 2025 wakati akipatiwa matibabu katika moja ya hospitali jijini Dodoma.
Taarifa ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliyoitoa imesema: “Kwa masikitiko makubwa, naomba kutoa taarifa ya kifo cha kiongozi wetu, mwanasiasa mkongwe na Spika mstaafu wa Bunge, Job Ndugai kilichotokea leo jijini Dodoma.
“Natoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na wananchi wa Jimbo la Kongwa, Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu.”
Dk Tulia amesema Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na kamati ya mazishi pamoja na familia ya marehemu inaratibu mipango ya mazishi na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.
Ndugai amefariki dunia akiwa na miaka 62. Alizaliwa Januari 21, 1963.