Job Ndugai afariki dunia, atakumbukwa kwa haya

Dodoma. Aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, amefariki dunia jijini Dodoma,

Taarifa ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, aliyoitoa leo Jumatano, Agosti 6, 2025, imesema: “Kwa masikitiko makubwa, naomba kutoa taarifa ya kifo cha kiongozi wetu, mwanasiasa mkongwe na Spika mstaafu wa Bunge, Job Ndugai, kilichotokea leo jijini Dodoma.”

“Natoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na wananchi wa Jimbo la Kongwa. Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu,” amesema.

Dk Tulia amesema Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na kamati ya mazishi pamoja na familia ya marehemu, inaratibu mipango ya mazishi na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.

Akitoa salamu za pole, Rais Samia Suluhu Hassan, amesema amepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Ndugai

“Ninatoa pole kwa familia, wanachama wote wa Chama cha Mapinduzi, watumishi wa Bunge na wabunge wote aliotumikia nao akiwa Spika wa Bunge letu, wananchi wa Kongwa, ndugu jamaa na marafiki.

“Tuungane pamoja kumuombea kwa Mwenyezi Mungu na kuwaombea familia, ndugu, jamaa na marafiki uvumilivu, faraja na moyo wa ibada katika kipindi hiki kigumu. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina,” ameeleza Rais Samia leo, katika taarifa kupitia mitandao ya kijamii.

Ndugai, aliyewahi pia kuwa Naibu Spika na Mwenyekiti wa Bunge, amefariki dunia akiwa na miaka 62. Alizaliwa Januari 21, mwaka 1963.

Amekuwa mbunge wa Kongwa tangu mwaka 2000, aliporithi kiti kutoka kwa Gideon Senyagwa ambaye hakugombea katika uchaguzi huo.

Katika mchakato wa kuwania ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu, Ndugai aliomba tena ridhaa ya CCM kuwania nafasi hiyo.

Katika matokeo yaliyotangazwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Kongwa, Joyce Mkaugala, kwenye kura za maoni ndani ya CCM, Ndugai aliongoza kwa kura 5,692, akifuatiwa na Isaya Mngurumi aliyepata kura 2,602.

Wengine na idadi ya kura walizopata kwenye mabano ni Deus Seif (1,260), Dk Samora Mshang’a (544), Dk Simon Ngatunga (517), Elias Mdao (435), Philip Chiwanga (558), Paschal Mahinyila (331), Balozi Emmanuel Mbennah (232) na Ngaya Mazanda (195).

Akiwa mbunge wa Kongwa baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, katika uchaguzi wa Spika wa Bunge la 12 uliofanyika Novemba 10, 2024, alishinda kwa kupata kura za ‘Ndiyo’ 344 kati ya kura 345 zilizopigwa, ukiwa ni ushindi wa asilimia 99.7. Alishika nafasi hiyo kwa miaka miwili.

Novemba 24, 2020, zikiwa zimepita siku 10 baada ya kuchaguliwa kuwa Spika, Ndugai aliwaapisha hadharani, nje ya ukumbi wa Bunge, wabunge 19 wa viti maalumu kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), licha ya kuwapo mzozo kwamba hawakupitishwa na chama hicho kushika nyadhifa hizo.

Waliapishwa nje ya ukumbi wa Bunge kwa kuwa kipindi hicho kulikuwa na tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19.

“Nitawalinda kwa namna yoyote ile, fanyeni kazi zenu za kibunge na kuwatumikia Watanzania, mimi nipo pamoja nanyi, msijali. Ninyi ni wabunge kama walivyo wengine,” alisema Ndugai.

Mzozo kuhusu nafasi za wabunge hao ulisababisha wavuliwe uanachama wa Chadema na kesi kufunguliwa mahakamani.

Kauli yake ya mwaka 2021 kuhusu Tanzania kuendelea kukopa kutoka nje ya nchi ilizua mjadala mpana, si tu bungeni bali pia katika jamii ya Watanzania kwa ujumla.

Kauli hiyo ilizua tafsiri tofauti miongoni mwa wananchi na viongozi, huku baadhi wakiona kuwa ilikuwa ni sauti ya tahadhari kwa mustakabali wa uchumi wa nchi, ilhali wengine waliiona kama kinyume cha msimamo wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Januari 6, 2022, Ndugai alitangaza kujiuzulu nafasi ya Spika wa Bunge, akieleza kuwa amefikia uamuzi huo kwa hiari baada ya kutafakari kwa kina. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Spika kujiuzulu kwa hiari katika historia ya Bunge la Tanzania tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Ndugai aliitisha mkutano na vyombo vya habari na akatumia sekunde 189 (dakika 3:09) kutoa kauli ya kuachia ngazi.

Alifikia uamuzi huo baada ya vuguvugu la siku 12 mfululizo, baada ya kauli yake kuhusu deni la Taifa aliyoitoa Desemba 26, 2021, kwenye mkutano wa Umoja wa Wagogo (Mikalile ye Wanyausi), alikozungumzia suala la kujitegemea kuliko kuwa tegemezi.

Katika hotuba hiyo, alitoa mfano wa Bunge lilivyopitisha sheria ya tozo kwenye miamala ya simu ili kupunguza utegemezi na madeni, kwani nchi ilishakopa sana kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Ndipo akasema: “Kuna wakati nchi itapigwa mnada” kama hatutakuwa makini katika kujitegemea.

Mwaka mmoja baadaye, Ndugai alimtaja Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela, kuwa ndiye aliyempa msukumo wa kujiuzulu. Alisema Mzee Malecela alimfuata nyumbani usiku wa Januari 5, 2022, na kumwomba aachie nafasi ya Spika wa Bunge.

Ndugai alisema haikuwa kawaida na hakuna siku ambayo Mzee Malecela aliwahi kuomba kuonana naye muda kama huo, lakini alipokea simu ya mkongwe huyo wa siasa nchini, akaomba kuonana naye nyumbani kwake Kongwa.

Walipokutana, alisema walizungumza kwa kifupi na kumshauri ajiuzulu kiti cha Spika, jambo alilolitekeleza siku iliyofuata.

Ndugai, mwanasheria, mwanasayansi na mtaalamu aliyebobea katika masuala ya uhifadhi, aliendelea kuwa mbunge wa Kongwa akishiriki siasa ndani ya CCM.

Aliendelea kutoa mchango mkubwa katika hoja za kibunge na ushauri kwa viongozi wenzake.