Kambi ya upasuaji wa mtoto wa jicho Iringa, mwanga mpya kwa maelfu vijijini

‎Iringa.Katika kuboresha huduma za afya ya macho kwa wananchi wa vijijini, kambi maalumu ya upasuaji wa mtoto wa jicho imeanzishwa Iringa kwa kushirikiana na Helen Keller International na Serikali kupitia Wizara ya Afya, ikilenga kutoa huduma kwa wagonjwa zaidi ya 700 walio hatarini kupoteza uwezo wa kuona.

‎Kambi hiyo inaendelea katika Kituo cha Afya cha Isimani, wilayani Iringa, ikiwa ni sehemu ya juhudi pana za kitaifa za kupunguza upofu unaozuilika na kurejesha uwezo wa kuona kwa wahitaji.

‎ ‎ ‎Akizungumza baada ya kufanyiwa upasuaji wa jicho,  Francis Mbambaga (51), mkazi wa kijiji cha Makuka, Wilaya ya Iringa, amesema alikuwa hawezi tena kufanya shughuli zake za kilimo kwa sababu ya upofu wa macho.

‎“Sikuamini kama ningeweza kuona tena hasa bure bila kulipia hata senti. Nashukuru sana kwa huduma hii,” amesema Francis.

Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa  Helen Keller International, Sarah Bouchie ameeleza kuwa kampeni hiyo inalenga kuwafikia watu wengi zaidi wanaoishi na mtoto wa jicho lakini hawana uwezo wa kupata huduma ya upasuaji.
‎ ‎
‎ “Tumekuwa tukifanya kazi nchini kwa zaidi ya miaka 40 tukisaidia vipaumbele vya Serikali katika maeneo matatu, kulinda uwezo wa kuona, kuboresha lishe na kutokomeza magonjwa yaliyopuuzwa ya tropiki (NTDs),” ameeleza Bouchie.

‎Ofisa Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho, Dk Greater Mande amesema mpango huu umesaidia kupunguza msongamano katika kliniki za macho na kuwafikia wagonjwa waliokuwa wakingoja kwa muda mrefu kupata matibabu.

‎”Gharama za kawaida za upasuaji wa mtoto wa jicho zinaweza kufikia hadi Sh300,000 kwa mgonjwa mmoja, hivyo huduma hii ya bure ni ya kubadili maisha,” amesema Dk Mande.

‎Dk Mande amesema kwamba kambi hizo huchangia vifaatiba na mahitaji mengine muhimu kwa hospitali na vituo vya afya vya wilaya, hivyo kuimarisha mfumo mzima wa utoaji huduma za afya.

‎ ‎Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James amesisitiza kuwa mkoa unathamini ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kuimarisha huduma za afya, hasa huduma za macho na magonjwa yaliyopuuzwa.

“Huduma za macho Iringa bado ni changamoto kutokana na upungufu wa wataalamu na wataalamu wabobezi wa macho,” amesema.
‎‎ ‎
‎Kwa niaba ya Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), William Lukuvi, amelipongeza Shirika la Helen Keller International kwa juhudi zake za kupambana na upofu unaozuilika, hususan mtoto wa jicho ambao ni moja ya sababu kubwa za upotevu wa uwezo wa kuona duniani.