Kocha Senegali hajaridhika, Mnigeria aingiwa na ubaridi

KOCHA Mkuu wa Senegal, Souleymane Diallo amesema licha ya timu hiyo kuanza vyema michuano ya CHAN 2024, ila haina maana wana kikosi bora cha kutetea tena taji hilo zaidi ya kuwaheshimu wapinzani wote wanaokutana nao kwa sasa.

Souleymane amesema hayo, baada ya timu hiyo kuanza kampeni za kutetea taji hilo kwa ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Nigeria katika pambano la Kundi D, lililopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.

“Kushinda kwetu imetuongezea morali kwa sababu kila mtu ameona jinsi ambavyo wapinzani wetu walikuwa bora katika kila upande, hii inaonyesha wazi tunapaswa kufanya zaidi ya hiki tulichokionyesha leo,” amesema Souleymane.

Kwa upande wa Kocha wa Nigeria, Daniel Ogunmodede amesema wamepoteza mechi ya leo kutokana na ubora na nidhamu iliyoonyeshwa na wapinzani wao.

“Kundi letu ni gumu na bado liko wazi kwa kila timu kusonga hatua inayofuata, tunahitaji kupambana zaidi kwa sababu ndio kwanza michuano imeanza na tumeona jinsi ambavyo washiriki wote walivyojipanga,” amesema.

Bao pekee la ushindi la Simba wa Teranga limefungwa na nyota wa timu hiyo, Christian Gomis dakika ya 75, akimalizia pasi safi iliyopigwa na Moctar Koita na kuanza vyema kampeni za kutetea tena ubingwa huo.

Senegal ndio watetezi wa michuano hiyo baada ya kuchukua taji hilo mwaka 2022, ilipowafunga wenyeji Algeria kwa penalti 5-4, kufuatia suluhu ya (0-0) katika dakika 120.