Kwa Mkapa badobado | Mwanaspoti

LICHA ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutangaza viingilio ni bure kwenye mechi za leo za mashindano ya CHAN, lakini Uwanja wa Mkapa hauna shamrashamra.

“Wanetu wa mzunguko watu 10,000 wa kwanza mnapata ofa ya tiketi ya kuingia uwanjani bila kulipa, unachotakiwa kufanya beba kadi yako ya N-Card suala la tiketi ya kuingia tuachie sisi  utaangalia mechi zote mbili,” ilieleza taarifa ya TFF muda mfupi uliopita.

Sasa wakati taarifa hiyo inaeleza hivyo, baadhi ya mashabiki  wamekuwa wakiingia uwanjani kwa kujivuta wakati mechi ya kundi B inayoendelea uwanjani hapo kati ya Burkina Faso na Afrika ya Kati.

Tofauti na mechi ya ufunguzi kati ya Tanzania na Burkina Faso ambayo kulikuwa na msongamano wa watu licha ya kuwa mechi hiyo kuwa na viingilio, lakini kwa sasa bado hakujachangamka.

Saa 2:00 usiku Tanzania itaikaribisha Mauritania kwenye mechi ya pili ya kundi B baada ya ule  wa kwanza wa Taifa Stars kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burkinafaso.