Makipa Taifa Stars wana jambo Chan 2024

MAKIPA wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Hussein Masalanga na Yakubu Suleiman wamezungumzia wanavyojifunza vitu vingi kupitia Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).

Masalanga ambaye anatarajia kuongeza mkataba mpya na Singida Black Stars baada ya ule aliokuwa nao kumalizika msimu uliopita, alisema michuano ya CHAN anaitumia kama fursa ya kujifunza vitu  vitakavyomsaidia katika Ligi Kuu Bara.

“CHAN inatukutanisha wachezaji kutoka mataifa mbalimbali na wenye viwango tofauti. Wapo ambao wana hatua kubwa ya mafanikio ya kisoka, hivyo tukibadilishana mawazo kuna kitu unakipata ukiwa na lengo la kujifunza,” alisema na kuongeza:

“Najifunza namna ambavyo wachezaji walivyo na mitazamo mikubwa kuhusiana na kufika mbali bila kukata tamaa, hadi michuano iishe kuna kitu nitakuwa nimetoka nacho, ila kubwa zaidi tuwaombe mashabiki wawe wanajitokeza kwa wingi kuja kutusapoti, kwani tupo aridhi ya nyumbani.”

Kwa upande wa Yakubu, kipa wa JKT Tanzania ambaye kwa sasa anatajwa huduma yake kuwaniwa na Simba alisema: “Kuna vitu vingi na vikubwa vya kujifunza kupitia CHAN hadi tutakaporejea kucheza Ligi Kuu tutakuwa tumeongeza kitu kipya.

”Jambo la msingi ni kujituma kuhakikisha Taifa Stars inafika mbali ikiwezekana kubakiza taji hilo nyumbani. Kwa pamoja tunaweza hivyo Watanzania wasichoke kutuunga mkono nyakati zote.”

Ukiachana na makipa hao aliyekuwa beki wa Simba, Yanga na Stars, Amir Mafhat alisema: “Michuano hiyo ni fursa kwa wachezaji vijana kujitangaza kimataifa, kuna wengine wanaweza wakabahatika kupata timu za kuzichezea maana soka ni biashara inayolipa.”