Moshi. Uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani 2025 umepangwa kufanyika Oktoba 29,2025 na tayari Chama cha Mapinduzi (CCM), kimetoa ilani yake ya uchaguzi (2025-2030), na moja ya kipaumbele ni kilio cha ajira nchini.
Lengo la CCM kupitia ilani hiyo, ni kuzalisha ajira zenye tija zisizopungua milioni nane katika sekta rasmi na isiyo rasmi na ili kufikia lengo hilo, kimeainisha mbinu 10 itakazozitumia kilio cha ajira kinachoelezwa ni bomu linalosubiri kulipuka.
CCM inatambua kuwa endapo kundi kubwa la vijana litakuwa nje bila kuwa na kazi, linaweza kuwa kiwanda cha kuzalisha mawazo ya uhalifu na ndio maana imekuja na mkakati huo, kama ilivyokuwa katika ilani yake ya 2020-2030.
Katika ilani hiyo (2020-2025), CCM ilifanikiwa kutengeneza ajira 8,084,203 katika sekta rasmi na isiyo rasmi na kati ya ajira hizo, sekta isiyo rasmi ilizalisha ajira 7,037,024 na sekta rasmi ajira 1,047,179 na hivyo kuvuka lengo la ilani hiyo.
Ripoti ya Ajira Rasmi na Kipato (Tanzania Formal Sector Employment and Earnings survey) iliyotolewa Julai 2025 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, inaonyesha Tanzania Bara na Zanzibar, ina wafanyakazi 4,073,887 walioko katika ajira rasmi.
Sekta Binafsi ndio ndio waajiri wakuu nchini ikiwa imeajiri wafanyakazi 2,853,566 katika sekta rasmi ikilinganishwa na watumishi 1,220,322 katika sekta ya umma.
Lakini takwimu za tovuti ya TICGL Data Driven Centre inaonyesha Tanzania, sekta isiyo rasmi inaongoza katika nyanja ya ajira ikiwa na asilimia 71.8 ya wafanyakazi, au takriban wafanyakazi milioni 25.95 wakijihusisha na kazi zisizo rasmi.
Tatizo la ajira kwa vijana ni la kidunia, takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO), zinaonyesha kiwango cha ukosefu wa ajira kwa mwaka 2023 kilikuwa asilimia 5.1, lakini kwa Tanzania, viwango vinatofautiana kulingana na chanzo cha habari.
Kwa mujibu wa Macrotrends, kiwango cha ukosefu wa ajira nchini Tanzania kwa mwaka 2023 kilikuwa asilimia 2.58 kikipungua kwa asilimia 0.01 ya mwaka 2022.
Hata hivyo, chanzo kingine kinaonyesha kiwango cha ukosefu wa ajira Tanzania kilikuwa karibuasilimia 8.8 kwa mwaka 2023, na kupungua kwa makadirio ya hadi asilimia 8.1 ifikapo mwaka 2030, Ilani ya sasa ya CCM itakapofika ukomo wake.
Lengo kuu la Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 ni kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa wananchi ambapo CCM itasimamia Serikali zake kutekeleza vipaumbele vinane ambavyo ni ni pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Ilani hiyo ilizinduliwa rasmi na mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, Jijini Dodoma Mei 30,2025 ambapo aliwakabidhi makamu wake wawili, mgombea mwenza, Dk Emmanuel Nchimbi, na mgombea urais Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.
Kwa mujibu wa wanazuoni mbalimbali wa Sayansi ya Siasa, Ilani ya uchaguzi ni ni nyaraka inayoweka sera na ahadi ambazo chama cha siasa kinatoa kuwa kitazitekeleza ikiwa kingeshinda uchaguzi mkuu kama ilivyo kwa Tanzania.
Katika Ilani hiyo ya uchaguzi mkuu kwa mwaka 2025-2030, CCM inatambua kuwa nyenzo kubwa ya kuwawezesha wananchi kuongeza kipato na kuondokana na umaskini ni kuongeza fursa za ajira kwa kuongeza shughuli za kiuchumi.
Hivyo, Chama kitaendelea kuisimamia Serikali kuhakikisha kuwa inakuza na kuwezesha shughuli za kiuchumi zinazoanzishwa na kuendeshwa na Watanzania ili kuwapa fursa ya kuendelea kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Ili kujenga mazingira ya kuongeza kipato na kupunguza umaskini, CCM itaweka mazingira sahihi ya kuzalisha fursa za ajira na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi hususan kwa makundi ya vijana, wanawake, watu wenye ulemavu, na wazee.
Lengo la Serikali ya CCM kwa mujibu wa ilani hiyo ya 2025-2030, ni kuzalisha ajira zenye tija zisizopungua 8,000,000 katika sekta rasmi na isiyo rasmi na inalenga kuona kuwa nusu ya ajira hizo zinazalishwa katika sekta rasmi nchini.
Katika kuendelea kupanua fursa za ajira kwa vijana na kuwawezesha wananchi kiuchumi, CCM imekuja na hatua za ziada 11 kwa lengo la kuielekeza na kuisimamia serikali kuchukua zitakazowezesha kufikiwa kwa lengo hilo.
Moja ni CCM itaielekeza na kuisimamia serikali kuanzisha na kutekeleza programu maalumu ya ujenzi wa miundombinu ya kongani (industrial sheds) za viwanda vidogo na vya kati vya kuongeza thamani ya mazao kwa kila mkoa na kila wilaya.
Serikali itaelekezwa kujenga angalau kongani moja ya viwanda kila mkoa ikilenga kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, uvuvi, ufugaji, misitu, madini na bidhaa za ujenzi kwa kuzingatia fursa za kijiografia katika mkoa na wilaya husika.
Katika kuwapunguzia wananchi gharama, serikali ya CCM itagharimia ujenzi wa kongani hizo pamoja na miundombinu muhimu kama vile barabara, maji, na umeme. Kazi ya mwekezaji mzawa itakuwa ni kununua na kuweka mashine husika.
Mbinu ya pili ni kuanzisha program maalumu kwa kushirikiana na sekta binafsi kuwawezesha wabunifu wanaoanzisha kampuni changa ikiwa ni pamoja na kuwapatia mitaji ya kuanzia, ujuzi, fursa za masoko na kuendeleza bunifu hizo.
Katika mbinu ya tatu, CCM kupitia ilani hiyo itaanzisha na dirisha maalumu kwa ajili ya mitaji ya kuanzisha kampuni changa kupitia Mfuko Maalumu wa kuwezesha upatikanaji wa Mtaji kwa wafanyabiashara wazawa wa Kitanzania.
Jambo la nne ni kuanzisha utaratibu maalumu kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutumia muda wao wa ziada kufanya kazi katika taasisi mbalimbali ndani na nje ya vyuo na tano ni kuanzisha maeneo maalumu ya uendelezaji wa bunifu na teknolojia zinazoibuliwa ili kuzalisha ajira nyingi hususan kwa kundi la vijana.
Vijana na uanzishaji makampuni
Mkakati wa sita ambao CCM itafanya ni kuweka mazingira wezeshi ya kisera na kimkakati kwa kuhamasisha uanzishwaji na kuimarisha makampuni ya vijana na Vyama vya Ushirika (SACCOS) vyenye kujiendesha kibiashara.
Hii itafanyika katika Halmashauri zote nchini ili yaweze kupata mikopo, mitaji na nyenzo kwa lengo la kuwezesha wananchi wengi zaidi wakiwemo wanaohitimu elimu ya juu na vyuo vya ufundi kujiajiri na kutoa ajira kwa wengine.
Katika mkakati wa saba, CCM imeahidi kuanzisha programu maalumu ya hamasa na mafunzo kwa Watanzania ili kutumia fursa za ajira nje ya nchi na nane ni kupitia upya mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kuwa na mfumo mmoja imara na uwezo wa kuhudumia makundi mbalimbali ya wananchi.
Mkakati wa tisa ili kuhakikisha ajira milioni 8 zinapatikana ni kuimarisha utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) ili kuibua na kutekeleza miradi ya kuzalisha ajira, kukuza uchumi wa kaya na kuendeleza rasilimali watu.
Mbinu ya 10 na 11 ni kuweka mazingira wezeshi ili kuchochea uanzishwaji na usajili wa makampuni ya kibiashara ili kurasimisha sekta isiyo rasmi na kuanzisha vituo vya mafunzo stadi kwa ajili ya kuandaaa vijana kushindana fursa za ajira nje.
Mhadhiri afunguka ajira milioni 8
Akizungumzia suala la ajira, mhadhiri Mwandamizi katika chuo cha Ustawi wa Jamii Jijini Dar es Salaam, Dk Riziki Nyello, alisema kutengeneza ajira zaidi ya milioni 8 inawezekana Tanzania, na kutaja sababu zinazowezesha hilo.
Dk Nyello alisema hiyo kwa mikakati ambayo Serikali inayo na kupitia Dira ya Taifa 2050, anaamini hata hizo ajira milioni 8 kwa miaka mitano zinaweza kuzidi.
“Moja ni mikakati iliyopo ya kuongeza thamani ya bidhaa tunazozalisha ambao kwenye Dira 2050 na kwenye mipango inayoandaliwa imewekewa msisitizo kwamba badala ya kupeleka nje bidhaa ghafi, ziongezewe thamani hapa nchini.”
“Mathalan hatusafirishi Parachichi nje kama parachichi, sasa kuna mikakati ya kuiongezea thamani hapahapa nchini kabla ya kuisafirisha nje. Maana yake hatupeleki ajira nje kwenda kwenye uchumi wa nchi zingine. Ni hapa hapa”
Dk Nyello alisema mkakati mwingine ni kuongeza mnyororo wa thamani ambayo mwisho wa siku huongeza ajira na kutolea mfano bidhaa za nyuki inavyoweza kuzalisha asali, gundi na mishumaa (organic candle) na kuongeza ajira.
Kwa mujibu wa mwanazuoni huyo, alisema ajira Tanzania sio chache bali kuna kutooana kati ya usambazaji wa ajira na mahitaji ya soko la ajira na kuhoji wale wanaoshia darasa la saba au kidato cha nne wanaandaliwaje kujiajiri.
“Hapa ndio maana unaona sera ya elimu imeboreshwa na kuja na suala la Amali ili akiishia la saba au kidato cha nne awe na ujuzi wa kujiajiri. Serikali inakwenda kutengeneza watu wenye ujuzi ambao watakwenda kuajiri wenzao,”alisema.
“Wakishaweza kujiajiri na kuajiri wengine hapa sasa inafuata hatua ya pili ya ajira zenye staha. Kwamba tayari huyu wa darasa la saba amekuwa fundi randa au mpiga rangi sasa linakuja sua;a la kuboresha ajira zilizotengenezwa”
Mkakati mwingine ni matumizi ya Tekinolojia kwamba nayo inaajiri watu wengi sasa na kutolea mfano kuwa mtu ana Parachichi kule Njombe lakini anaweza kumuuzia mtu aliyepo Dar es Salaam na kuibua uchumi wa kidigitali.
Dk Nyello alisema hiyo inaenda kuzalisha watu wa kati (middlemen) ambao wao hawana bidhaa lakini ana simu janja anasimama kuuza bidhaa ya mtu mwingine na hao ni wengi wako kwenye mitandao wakiuza bidhaa ambazo sio zao.