Mambo saba yaliyobeba Ilani ya ACT Wazalendo

Dar es Salaam. Uchumi wa watu, kuboresha huduma za jamii kwa wote na miundombinu bora kwa uchumi na ustawi wa wananchi ni miongoni mwa mambo yaliyomo kwenye Ilani ya ACT Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyia Oktoba 29, 2025.

Mengine ni kujenga taifa lenye haki na demokrasia ili kuondoa rushwa na kujenga Serikali yenye uwazi na uwajibikaji, kulinda na kusimamia ardhi, mazingira na rasilimali kwa maslahi ya wananchi wote.

Mwenyekiti wa kamati ya Ilani ya uchaguzi ya ACT Wazalendo, Emmanuel Mvula amesema hayo wakati akiwasilisha muhtasari wa yaliyomo kwenye ilani itakayopitishwa leo Jumatano Agosti 6, 2025 na wajumbe wa mkutano mkuu maalumu unaondelea katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Kabla ya kuwasilisha muhtasari huo, Mvula amewahakikishia wajumbe wa mkutano huo kuwa ilani hiyo ya uchaguzi imebeba maono ya kujenga Tanzania mpya itakayokuwa na maslahi ya wote na manufaa kwa wote.

“Tumejipanga kuhakikisha uchumi unakuwa kwa watu na si takwimu, huduma za jamii zinatekelezwa kwa haki na miundombinu inajengwa kwa maendeleo ya watu si kwa sifa za kisiasa,” ameeleza Mvula.

Amesema endapo ACT Wazalendo ikifanikiwa kushika madaraka itahakikisha inazalisha uchumi wa watu utakaozalisha ajira milioni 12 kupitia viwanda, kilimo, uvuvi, mifugo, biashara, sanaa na huduma za teknolojia.

“Serikali ya ACT Wazalendo itawezesha kwa kiwango kikubwa maeneo ya uwekezaji na kuwezesha wananchi kiuchumi,” amesema Mvula.

Kuhusu kuboresha huduma za jamii kwa wote, Mvula amesema ilani ya ACT Wazalendo itakuwa na mkakati maalumu wa kutoa huduma bora za afya, elimu, maji na nishati na hifadhi ya jamiina watawekeza bima ya afya kwa wote.

“Tutatoa huduma za kutosha kwa watumishi wa elimu na kada ya afya.

Amesema ACT Wazalendo imedhamilia kuboresha miundombinu ili kuchochea maendeleo ya uchumi na kijamii kwa kujenga reli ya kisasa ya SGR kanda ya kusini sambamba na kujenga barabara za kimkakati.

“Tutapambana na vitendo na ukandamizaji na uonevu dhidi ya vyombo vya dola, polisi itakuwa huduma kwa jamii si badala ya kutumia nguvu dhidi ya wananchi Tutajenga mifumo bora ya haki jinai na ndani ya miezi sita ya kwanza tutafufua mchakato wa Katiba Mpya ya wananchi, ” amesema Mvula.