TIMU ya Mashujaa FC imeweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya jijini Dar es Salaam huku ikiwa na sura tisa mpya.
Mwezi uliopita timu hiyo ilitangaza kuachana na wachezaji tisa ambao ni Ibrahim Ame, Yahya Mbegu, Jeremanus Josephat, Emmanuel Martin, Ibrahim Nindi, Zuberi Dabi, Omary Kindamba, Abrahman Mussa, Ally Nassor na Mohamed Mussa.
Ili kuziba nafasi zilizo wazi Mashujaa imesajili wachezaji wengine wapya katika nafasi za ulinzi, kiungo na ushambuliaji.
Wachezaji watatu tayari wametambulishwa akiwamo Ismail Mgunda kutoka AS Vita ya DR Congo, Frank Magingi aliyekuwa akikipiga Geita Gold na Mudathir Said ambaye ametokea Mbeya City ilhali wengine sita wanaendelea kusubiri kutangazwa.
Katibu wa timu hiyo, Edward Swai alisema wachezaji wameanza kambi ya muda iliyopo Kunduchi wakijiandaa kabla ya kwenda Arusha ambako wataweka kambi.
“Dar ilikuwa ni makutano, lakini mwalimu ameamua kuanzia programu zake wakati taratibu zingine zikiendelea. Tunategemea kama awali ilivyokuwa timu iende Arusha, lakini ikitokea mabadiliko yoyote pia tutawajulisha,” alisema Swai.
Aliongeza kwamba usajili umefanyika kwa matakwa ya kocha kutokana na mapendekezo yake na wanaamini kwamba ushirikiano kati ya wachezaji wapya na wale waliopo utaisaidia timu hiyo kufikia malengo.
Ligi Kuu Bara msimu ujao inatarajiwa kuanza Septemba 16, mwaka huu.