Dar es Salaam. Huenda mfumo wa haki jinai nchini ukapitia mageuzi makubwa, iwapo pendekezo la Chama cha Mapinduzi (CCM) la kuanzishwa kwa Ofisi ya Kitaifa ya Upelelezi (NBI) litatekelezwa.
Hatua hiyo, kwa mujibu wa wadau wa kada mbalimbali, inaweza kubadilisha mfumo wa utoaji wa haki nchini na kuleta sura mpya kwa majukumu ya Jeshi la Polisi.
Pendekezo hilo ni sehemu ya ahadi za CCM, katika Ilani yake ya Uchaguzi ya 2025/30, ikieleza ofisi hiyo itakuwa huru na itatekeleza jukumu la upelelezi wa makosa ya jinai kutoka kwa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (CID), ambayo kwa sasa ipo chini ya Jeshi la Polisi.
“Kuanzishwa kwa mamlaka mpya na huru ya upelelezi itakayojulikana kama Ofisi ya Kitaifa ya Upelelezi, itakayowajibika kwa uchunguzi wa makosa yote ya jinai,” inasomeka sehemu ya ilani hiyo, ukurasa wa 40.
Akizungumza hivi karibuni kwenye jukwaa la Café Talk, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Ally Hapi alisema kwa sasa upelelezi wa makosa ya jinai unafanywa ndani ya Jeshi la Polisi, ambapo Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP).
“Tunataka kutenganisha majukumu haya kwa kuanzisha taasisi ya upelelezi iliyo huru, yenye bajeti yake na uwezo wa kufanya kazi bila kuingiliwa sawa na jinsi FBI ya Marekani inavyofanya kazi,” alisema.
Ingawa wengi wanaona wazo hilo kama hatua chanya ya kitaasisi na kitaaluma, wataalamu wa sheria wanaonya utekelezwaji wa hilo, lazima uambatane na mageuzi mapana zaidi ya mfumo wa haki jinai.
Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Harold Sungusia aliunga mkono wazo hilo, akisema limechelewa kwani lilipaswa kutekelezwa kitambo.
“Tumekuwa na ucheleweshaji mkubwa wa kuanzisha NBI. Kuna mapendekezo mengi yaliyotolewa na Tume ya Rais kuhusu Mageuzi ya Haki Jinai chini ya Jaji Othman Chande, hili ni mojawapo tu. Ni tiba ya awali, lakini maradhi ni mengi,” alisema.
Sungusia alifafanua mfumo wa haki jinai una sehemu 11 zinazoingiliana kuanzia hatua ya kuzuia uhalifu, uchunguzi, kushtaki, hadi urejeaji wa wahalifu na kuzuia wasirudie makosa.
“Sehemu moja ikiwa dhaifu, mfumo mzima unalegalega,” alisema Sungusia.
Miongoni mwa mapendekezo yake, Sungusia alisisitiza hitaji la kulibadili Jeshi la Polisi kutoka mfumo wa kikoloni na kulifanya kuwa huduma ya usalama inayolenga jamii.
Alihimiza jeshi hilo ligatuliwe na kuwekwa chini ya mamlaka za serikali za mitaa, ili kuunda polisi wa wananchi watakaoshirikiana na mipango ya maendeleo ya miji.
Pia alipendekeza kuundwa kwa taasisi huru ya kusimamia Jeshi la Polisi, kama ilivyo Kenya au Afrika Kusini, kwa ajili ya kutoa uwajibikaji na kushughulikia ukiukwaji wa maadili ndani ya jeshi hilo.
Zaidi, alitaka mageuzi hayo yalingane na taasisi zilizopo. Kwa maoni yake, NBI ilipaswa kuanzishwa sambamba na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, inayoongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
“Naamini kuchelewa kwa NBI ni kwa sababu ilipaswa kuanzishwa pamoja na NPS, kama ilivyo nchini Uingereza ambapo Shirika la Kitaifa la Uhalifu (NCA) hufanya kazi sambamba na Ofisi ya Mashtaka ya Umma,” alisema.
Wananchi mbalimbali jijini Dar es Salaam, wameonyesha matumaini, wengi wakiamini kuwa NBI inaweza kusaidia kasi ya uchunguzi na kutoa majibu ya kweli, hasa kwenye kesi za ufisadi na zinazovuta hisia za umma. “Mara nyingi tunasikia kesi zinasuasua kwa sababu ya kuingiliwa kisiasa. Labda chombo huru kinaweza kufanya kazi bila kuogopa,” amesema mfanyabiashara wa Dar es Salaam, Rashid Juma. Wengine wameelezea hofu kuhusu gharama za uendeshaji na kama taasisi hiyo mpya haitarudia makosa ya zile zilizopo sasa.
Wanaounga mkono wazo hilo, wanadai taasisi huru kama NBI italeta weledi, haki na kuaminika zaidi, hasa katika kesi zenye uzito au zinazogusa masuala ya kisiasa na ufisadi.
Pendekezo hili linakuja baada ya miaka mingi ya malalamiko kutoka kwa asasi za kiraia na vyama vya upinzani kwamba baadhi ya uchunguzi huchakachuliwa kutokana na ushawishi wa kisiasa.
Hata hivyo, maswali mengi bado hayajajibiwa kuhusu namna ofisi hiyo mpya itakavyofanya kazi. Haijajulikana iwapo NBI itaanzishwa kwa sheria mahususi ya Bunge na kama mamlaka yake yatahusisha tu makosa makubwa kama ufisadi, ugaidi na uhalifu uliopangwa, au itashughulikia pia kesi za kawaida.
Kuna mashaka pia kama Tanzania ina rasilimali watu za kutosha kuendesha taasisi ya kiwango cha juu kama hiyo.
Zaidi, haijafahamika itakuwaje NBI itagawana majukumu bila kugongana na Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mashtaka.
Maofisa wa polisi, ambao hawakutaka majina yao yatajwe, waliunga mkono mageuzi hayo kwa ujumla, lakini walionya kuwa majukumu yanayofanana huenda yakasababisha mivutano ya mamlaka.
“Kama sheria haitabainisha kwa uwazi nani afanye nini, basi kutakuwa na mkanganyiko,” alisema ofisa mwandamizi wa polisi.
Nchi kama Kenya, yenye Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) iliyo chini ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi na Marekani yenye FBI inayojitegemea, ni mifano ambayo Tanzania inaweza kujifunza. Lakini wataalamu wanaonya, uhuru peke yake si suluhisho.