Mkenya anukia Pamba Jiji | Mwanaspoti

MABOSI wa Pamba Jiji wako katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa kiungo raia wa Kenya, Saphan Siwa Oyugi baada ya nyota huyo aliyejiunga na Kagera Sugar dirisha dogo la Januari 2025 kumaliza mkataba.

Siwa alijiunga na Kagera Sugar iliyoshuka msimu uliopita kutoka Ligi Kuu Bara hadi Championship, ambapo alitua kwa mara ya kwanza ili kutafuta changamoto mpya baada ya mkataba wake na Tusker ya Kenya kumalizika.

Taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata zinaeleza kuwa sababu kubwa ya Pamba kuiwinda saini ya nyota huyo ni kutokana na kocha mpya wa kikosi hicho Mkenya Francis Baraza kumtaka akiwataka mabosi wa timu hiyo kukamilisha dili hilo mapema.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Pamba, Ezekiel Ntibikeha alisema kinachoendelea kwa sasa ni tetesi tu na sio uhalisia, ingawa baada ya kukamilisha taratibu zote wataanza kutangaza usajili wa mastaa wapya watakaokuwa nao.

“Usajili tunaofanya ni mkubwa na tunaamini utaleta manufaa makubwa. Siwezi kusema ni wachezaji gani tumenasa saini zao hadi sasa, ila niwahakikishie mashabiki wetu watafurahia tutakapoanza tu kuwatangaza,” alisema.

Nyota huyo kabla ya kujiunga na Kagera Sugar alikuwa anaongoza kwa wachezaji wenye asisti nyingi katika Ligi Kuu Kenya, ambapo alikuwa nazo tisa, huku katika Ligi Kuu Bara alipokuwa na ‘Wanankurunkumbi’ aliwafungia bao moja.

Bao hilo alifunga katika mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo Kagera ilishinda 2-1 dhidi ya Pamba Jiji, Machi 7, 2025, ambapo pambano la miamba hiyo lilipigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba uliopo Bukoba.