Dar es Salaam. Kada mpya wa ACT Wazalendo, Luhaga Mpina na Aaron Kalikawe wamependekezwa na halmashauri kuu ya chama hicho iliyoketi jana Jumanne Agosti 5, 2025 kuwania urais wa Tanzania.
Wakati Mpina na Kalikawe wakipendekezwa kuwania urais wa Tanzania, Jina la Mwenyekiti wa chama hicho, Othman Masoud ndio pekee pia lililopendekezwa kugombea urais wa Zanzibar.
Majina haya yote leo Jumatano Agosti 6, 2025 yanapigiwa kura na kuthibitishwa katika mkutano mkuu wa ACT Wazalendo utakaofanyika baadaye katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano wa ACT Wazalendo, Shangwe Ayo imeeleza halmashauri kuu imeridhia Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu aliyetiania kuwania urais, kujitoa katika mchakato huo.
“Semu alieleza halmashauri kuu kuwa amechukua hatua hiyo, katika kutekeleza wajibu wake wa kiuongozi ili kukiwezesha chama kutekeleza wajibu wa kimapambano ya kuiondoa CCM madarakani kwenye Uchaguzi Mkuu 2025, kwa kuzingatia mazingira ya kisiasa ya sasa nchini,” amesema Shangwe.
Ingawa taarifa ambazo Mwananchi inazo zinaeleza haikuwa rahisi Semu kufikia uamuzi huo kwa kuwa alishajiandaa kuwania urais katika uchaguzi wa Oktoba akipeperusha bendera ya ACT Wazalendo.
Katika vikao vya jana Jumanne asubuhi ulitumika ushawishi mwingi na mvutano wa hapa na pale kuanzia kamati ya uongozi yenye mamlaka ya juu hadi kamati kuu, ili kumlainisha Semu ajiondoe kwenye mchakato huo.
Awali, chanzo cha habari kilieleza Semu aligoma kujiondoa kuwania nafasi hiyo kwa Mpina aliyewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, kadhalika alikuwa tayari hata kusimama naye katika kura za maoni za ndani ya chama hicho
Hata hivyo, viongozi hawakukubaliana na hatua ya Semu kutaka kuingia kwenye kura za maoni na Mpina kuhofia aibu itakayoweza kujitokeza endapo angepata kura chache, ndio walifanya jitihada jambo limalizike hatua ya chini bila kufika mkutano mkuu.